Thursday, August 16, 2012
BADO TUNA NIA YA KUILETA REAL MADRID, BARCA - RAIS KIKWETE
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa bado ni dhamira ya Serikali yake kuileta moja ya timu za Ligi Kuu ya Soka ya Hispania (La Liga) kutembelea Tanzania na amemtaka Balozi mpya wa Hispania katika Tanzania kusaidia kufanikisha dhamira hiyo.
Aidha, Rais Kikwete ameipongeza Hispania kwa kutetea ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro) 2012 katika mashindano yaliyomalizika mwezi uliopita nchini Poland na Ukraine.
Akizungumza na Balozi mpya wa Hispania, Mheshimiwa Luis Manuel Cuesta Civis mara baada ya kupokea hati yake ya utambulisho katika hafla fupi iliyofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais alisema: “Wananchi wa Tanzania, ambako timu za Hispania, zina washabiki na wafuasi wengi, bado wanasubiri kwa hamu ziara ya moja ya timu kubwa za Ligi Kuu ya Soka ya Hispania. Tunataka ije hapa, icheze mechi moja ama mbili na itembelee mbunga zetu maarufu za wanyama,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kama utakavyokuja kuthibitisha mwenyewe, Watanzania ni watu wanaopenda michezo na hasa soka na ni wafuatiliaji wakubwa wa Ligi Kuu ya Hispania ambako timu zenye mvuto zaidi ni Real Madrid na Barcelona.”
Rais Kikwete pia aliipongeza Hispania kwa kutetea ubingwa wake wa Ulaya.
“Tunawapongeza sana kwa kuweka historia. Kwanza mlishinda Kombe la Mataifa ya Ulaya, kisha mkashinda Kombe la Dunia. Sasa mmeweza kutetea Kombe la Ulaya. Hili halijapata kutokea kwa nchi moja kushikilia vikombe vyote viwili vikubwa vya soka duniani kwa wakati mmoja ama nchi kutetea Kombe la Ulaya.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment