Aggrey Morris akiongoza msafara wa wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati wakiwasili kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana. |
Akizungumza na wanahabari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana baada ya Stars kuwasili ikitokea Botswana kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa hilo, Kim alisema kwamba timu yake ilicheza vizuri katika dakika zote 90 lakini inahitaji mechi zaidi zitakazowafanya wachezaji kuzoeana zaidi.
Katika mechi hiyo ya kirafiki, Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ilitoka sare ya kufungana mabao 3-3 na The Zebras ya Botswana hivi kuacha gumzo kubwa katika mitaa ya Gaborone kwani wengi walitarajia timu yao kuibuka na ushindi.
“Timu ilicheza vizuri, ndani ya dakika 90 ingawa kulikuwa na makosa madogo katika safu ya ulinzi yaliyosababishwa na kasi ya ushambuliaji ya wapinzani wetu,” alisema Poulsen.
Poulsen alisema kwamba idadi kubwa ya vijana waliopo ndani ya timu hiyo ndiyo chachu ya mafanikio ya timu kwa sababu soka hivi sasa inachezwa na vijana.
“Nimevutiwa sana na ushirikiano wa Haruna Moshi (Boban) na Mrisho Ngassa, na hata baadaye alipoingia Simon Msuva pia alionyesha kucheza vizuri sana na Ngassa... ukiangalia goli la tatu lililofungwa na Ngassa unaona ilikuwa ni kazi nzuri iliyofanywa na Msuva,” alisema Poulsen.
“Katikati kulikuwa na ushirikiano mzuri wa Athuman Iddi 'Chuji' na Shaban Nditi, waliwamudu wapinzani wetu, Mwinyi Kazimoto na Frank Damayo pia walionyesha uwezo mkubwa... hii ndiyo sababu inayonifanya niseme kwamba hivi sasa timu iko vizuri vijana wanatambua wajibu wao wanacheza soka la kuelewana, hawana ubinafsi wala hawabutui na hawakimbii ovyo na mpira.”
Akizungumzia wapinzani wake, Poulsen alisema kwamba Zebras ni timu nzuri sana wanacheza mpira unaoeleweka kwa sababu wamekaa kambini muda mrefu na maandalizi yao ni makubwa sana ukilinganisha na Stars, wanacheza mechi nyingi za kimataifa katika viwanja tofauti, na ndiyo maana amevutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na Stars kwani vinginevyo wangefungwa magoli mengi sana katika mechi hiyo.
“Wapinzani wetu wanacheza soka la uhakika kwa sababu wamekaa pamoja. Timu isipopata muda wa kukaa pamoja na kucheza mechi nyingi za kimataifa ndani na nje ya nchi haiwezi kufanya vizuri katika mashindano yoyote.”
Alitumia muda huo pia kuwashukuru wadhamini, Kilimanjaro Premium Lager na kusema sasa hivi mambo yanaenda vizuri kwani timu ina uwezo wa kufanya mipango ya muda mrefu kutokana na kuwa na mdhamini wa uhakika.
Naye Nohodha wa timu hiyo Juma Kaseja alisema kwamba timu ni nzuri ingawa imesheheni vijana ambao bado wanakumbwa na woga wa kucheza mechi za kimataifa lakini wakipewa nafasi ya kucheza mechi nyingi za kirafiki hususan mechi za nje kama hii waliocheza itazidi kuwajenga zaidi.
“Imefika wakati sasa timu ya taifa ipewe umuhimu, sio timu isubiri mechi ambazo ziko kwenye kalenda ya FIFA tu... timu itafutiwe mechi nyingi wakati wowote, ili wachezaji wazidi kukaa pamoja kwa muda mrefu, wapate uzoefu, hilo lisipozingatiwa hakuna hatua yoyote tutakayopiga,” alisema Kaseja.
Kambi ya timu hiyo tayari imevunja na wachezaji wanarejea kwenye klabu zao kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.
No comments:
Post a Comment