Friday, August 17, 2012

HATIMAYE VAN PERSIE ASAINI MIAKA MINNE MAN UNITED, FERGIE ASEMA RVP ALITAKA "MNO" KUJA OLD TRAFFORD

Robin van MAGOLI.... sasa mtanikoma

LONDON, England
MCHEZAJI wa kimataifa wa Uholanzi, Robin Van Persie "alikuwa akitaka mno" kujiunga na Manchester United na alitaka changamoto ya "kuja kwenye klabu kubwa zaidi duniani", kocha Alex Ferguson amesema leo, baada ya kukamilisha usajili wa nahodha huyo wa zamani wa Arsenal.

Van Persie, msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England baada ya kufunga magoli 30, amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga Man United leo baada ya kusaini miaka minne.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alikuwa pia akihusishwa vikali na mabingwa wa England, Manchester City baada ya kutangaza Julai kwamba hataongeza mkataba wa kuichezea Arsenal, uliokuwa umalizike 2013.

"Haikuwa rahisi," Ferguson aliiambuia MUTV.

"Inafahamika kwamba (kocha wa Arsenal) Arsene Wenger hakutaka kumuuza kwa Manchester United. Kijana mwenyewe alikuwa akitaka kuja kwetu na jambo hilo ndilo lililokuwa muhimu.

"Alikataa ofa za klabu kibao ili kujiunga nasi kwa sababu alitaka changamoto ya kuchezea klabu kubwa zaidi duniani. Nadhani jambo hilo ni baa'kubwa.

"Hicho ndicho kilichofanya jambo hilo (la kutua Man United) liwezekane... maafikiano pekee yaliyobaki yakawa ni kuhusu ada ya uhamisho na Arsenal kwa sababu hapakuwa na kikwazo tena kwavile kijana alitaka sana kuja Manchester United."

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Man United imelipa paundi milioni 24, na Van Persie, ambaye alifunga jumla ya magoli 132 katika mechi 278 alizoichezea Arsenal tangu alipojiunga akitokea Feyenoord mwaka 2004, anajiandaa kucheza mechi yake ya kwanza kwa Man United katika Ligi Kuu ya England dhidi Everton Jumatatu.

Ferguson alisema fursa ya kumsajili mchezaji wa kiwango cha Van Persie ilikuwa ni ngumu sana kwao kujizuia kuichangamkia.

"Sikufikiria kama ingewezekana kumsajili van Persie wakati tulipomzungumzia mwaka jana lakini, niliposikia kwamba amekataa kusaini mkataba mpya na akaweka hadharani kwamba anataka kuondoka Arsenal, hapo tukaona tuchangamkie - hakuna maswali kuhusu hilo.

"Robin ni mshambuliaji wa kiwango cha dunia mwenye rekodi inayothibitisha England na Ulaya.

"Kipaji chake hakihitaji kutambulishwa kwa mashabiki wetu - amefunga magoli mengi dhidi yetu katika mechi kali akiwa na klabu yake ya zamani. Anavyojua kujipanga, umaliziaji na uwezo wake kwa ujumla uwanjani ni baab'kubwa."

Licha ya kuwa na msimu wa kutisha, Van Persie aliiambia Arsenal mwezi uliopita kwamba hakuwa na furaha na mwelekeo wa klabu hiyo.

Arsenal, ambao walimaliza wa tatu katika Ligi Kuu ya England msimu uliopita, hawajatwaa ubingwa wowote tangu mwaka mwaka 2005 walipotwaa Kombe la FA.

"Ni heshima kubwa kujiunga na Manchester United," Van Persie aliiambia tovuti ya Man United (www.manutd.com).

"Hivi sasa najiandaa kufuata nyayo za washambuliaji wengi wakubwa, kuleta uzoefu wangu na kutoa mchango wangu katika kuisaidia timu kupigania makombe makubwa. Nina hamu sana ya kushuka uwanjani."

Man United walinyang'anywa kombe lao kwa tofauti ya magoli dhidi ya mahasimu wao wa mji mmoja Man City wakati kikosi cha kocha Roberto Mancini kilipotwaa ubingwa katika siku ya mwisho ya ligi iliyojaa 'drama'.

No comments:

Post a Comment