*KAFULILA, MACHALI WAWASHA MOTO
*KANUNI ZATUMIKA KUZIMA MJADALA
Mitambo ya kufua umeme ya Dowans |
Mhe. Moses Machali |
Mhe. David Kafulila |
Mwanasheria Mkuu, Fredrick Werema akifafanua jambo bungeni. Anayemtazama ni Mhe. Lukuvi |
LILE sakata la serikali kutakiwa kulipa malipo ya mabilioni
ya pesa kwa kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba wa kampuni hewa ya kufua umeme
ya Richmond limeibuka upya bungeni asubuhi hii na kuibua malumbano makali
bungeni kati ya Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Sylvester Mabuma, Waziri wa Nchi
katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) , Mhe. William Lukuvi na wabunge Mhe. Moses Machali na
Mhe. David Kafulila.
Tukio hilo lililoibuka leo asubuhi baada ya kipindi cha
maswali na majibu, lilianzia kwa Mhe. Machali, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi)
, ambaye alisimama na kutumia kanuni ya 68 (7) kuomba mwongozo wa spika
kuhusiana na madai aliyotoa awali Kafulila kuwa anao ushahidi kwamba serikali itashindwa
katika kesi inayoikabili dhidi ya Dowans.
Hata hivyo, kabla Mhe. Machali hajamaliza kueleza kile
alichotaka apewe mwongozo wake, akasimama Mhe. Lukuvi na kuomba atoe taarifa. Waziri huyo
akasema kuwa kwa mujibu wa kanuni, kifungu cha 68(1), Machali hapaswi kuomba
mwongozo kwa vile wakati akisimama hakukuwa na msemaji mwingine aliyekuwa
akizungumza kama kanuni inavyoelekeza.
Baada ya hapo, Mhe. Machali naye akasimama na kutaka kutoa
taarifa.
Mwenyekiti Mabuma akamzuia na kumtaka asubiri Mhe. Lukuvi amalize
anachosema ndipo atakapopewa nafasi. Kitendo hicho kikaonekana kumkera Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), Mhe.
Kafulila ambaye naye alisimama bila kusubiri ridhaa ya kiti na kuhoji ni
kwanini Mwenyekiti anamruhusu Mhe. Lukuvi kumkatisha Mhe. Machali lakini,
wakati huohuo anamzuia Machali kutoa taarifa yake.
Hapo mwenyekiti akawa mkali na kumtaka Mhe. Kafulila akae na
kuheshimu kanuni inayomtaka kila mmoja kuzungumza baada ya kupata ridhaa ya kiti.
Baadaye Mhe. Mabuma akampa ruhusa Machali kuendelea na maelezo yake ya kuomba mwongozo kwa kusema kuwa ameitumia kwa usahihi kanuni ya 68(7) na sio aliyodai Lukuvi ya 68(1).
Baadaye Mhe. Mabuma akampa ruhusa Machali kuendelea na maelezo yake ya kuomba mwongozo kwa kusema kuwa ameitumia kwa usahihi kanuni ya 68(7) na sio aliyodai Lukuvi ya 68(1).
DOWANS
Aliposimama tena, Mhe. aMachali akaomba mwongozo wa kiti
kuhusu maelezo aliyotoa Mhe. Kafulila bungeni hapo, kuwa anao ushahidi kwamba
Serikali itashindwa kesi yake dhidi ya Dowans na hivyo italipa mabilioni ya
pesa za walipa kodi.
Mhe. Machali akaomba mwenyekiti amtake Kafulila awasilishe taarifa
sahihi za ushahidi wa yale aliyotamka ili ikibidi hatua stahiki zichukuliwe kwa
nia ya kuliokoa taifa na uwezekano wa kupoteza fedha nyingi.
Hata hivyo, kabla mwenyekiti hajatoa mwongozo wake,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Fredick Werema alisimama na kutaka
wazungumzaji watambue kuwa suala la Dowans liko mahakamani na hivyo, kwa mujibu
wa kanuni ya 64 (c) ya Bunge, kamwe halipaswi kujadiliwa.
Kwa maelezo hayo, Werema akaomba matakwa ya kanuni
yazingatiwe na kwamba, kama mbunge (Mhe. Kafulila) anao ushahidi wowote kuhusu
jambo hilo, basi aupeleke mahakamani.
Mwenyekiti aliposimama, aliungana na Mwanasheria Mkuu na kusema
kuwa ni lazima kanuni zizingatiwe na hivyo, kama Mhe. Kafulila ana ushahidi
wowote kuhusiana na Dowans aupeleke mahakamani na kwa kufanya hivyo atakuwa
ameisaidia sana mahakama.
No comments:
Post a Comment