WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAMKO
LA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI KUHUSU MGOGORO ULIOWASILISHWA NA CHAMA
CHA WALIMU TANZANIA (CWT)
Serikali kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu
kiongozi ilipokea notisi ya saa 48 ya kusuduio la wanachama wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT) kugoma Kuanzia Jumatatu tarehe 30.07.2012. Notisi hii ilipokelewa Ijumaa tarehe 27/07
saa 9 alasiri. Mgogoro huo unaelezwa na CWT kuwa unatokana
na Serikali kushindwa kutimiza madai ya Walimu ambayo wameyataja kuwa ni:
i.
Nyongeza ya mshahara ya asilimia 100 kwa
walimu wote nchini;
ii.
Kulipwa posho ya kufundisha kwa walimu wa
sayansi asilimia 55 na walimu wa sanaa asilimia 50; na
iii.
Kulipwa posho ya mazingira magumu asilimia
30 kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
2.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Mgogoro huu ulisajiliwa Tume ya Usuluhishi
na Uamuzi (Commission for Mediation and
Arbitration – CMA). Tarehe 26 Juni, 2012,
kikao cha kwanza cha usuluhishi kati ya CWT na Serikali kilifanyika chini ya
Msuluhishi wa Tume. Katika Kikao hicho
ilikubalika kuwa CWT iandae na kuwasilisha hati ya ufafanuzi wa madai yake na
Serikali itoe majibu kabla au ifikapo tarehe 9 Julai, 2012.
Kikao cha pili cha usuluhishi kilifanyika
tarehe 10 Julai, 2012 kama ilivyopangwa na pande zote mbili zilitimiza matakwa
ya Msuluhishi. CMA iliomba serikali iwasilishe mapendekezo (offer) ya kiwango
ambacho inaweza kukiongeza kwa kuzingatia madai ya CWT. CMA ilipendekeza
majadiliano yaendelee tarehe 20/07/2012.
Tarehe 20/07/2012 serikali
iliwasilisha mapendekezo (offer) kuwa imeongeza mshahara wa walimu kwa wastani
wa asilimia 14 tofauti na watumishi wengine ambao wamepata nyongeza ya wastani
wa asilimia 13 kiwango ambacho kilifikiwa katika mjadala wa nyongeza za mishahara
ya watumishi wa umma (Public Service Joint Staff Council) ambao CWT ni wajumbe
na walihudhuria. Nyongeza hiyo ya walimu imetokana na utaratibu wa serikali wa
kuboresha mishahara kwa watumishi wa umma. Vilevile, Serikali ilitoa taarifa
kuwa imeunda Bodi ya Mishahara na Maslahi kwa ajili ya kumshauri Mhe. Rais juu ya misingi ya mishahara katika
utumishi wa umma. Bodi imeanza kazi tarehe 01 Julai 2012 na inahitaji muda wa
kufanya kazi na kuja na mapendekezo ambayo yatatumika kuboresha mishahara na
maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo walimu. CWT walikataa mapendekezo (offer)
hayo na Msuluhishi alitoa uamuzi wa kushindwa kusuluhisha mgogoro huo na
kuziomba pande zote mbili kufika Tume tarehe 25/07/2012 kwa ajili ya kuchukua
cheti cha uamuzi kushindwa kusuluhisha (certificate of Deadlock).
Baada ya Serikali kutafakari athari za mgomo
na kwa kuzingatia kuwa Chombo ambacho kilipaswa kupokea na kujadili madai ya
CWT ambacho ni “Teachers Service Joint Staff Council” hakikuwepo. Tarehe 26 Julai 2012 Serikali iliwasilisha
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi maombi ya
kuzuia mgomo pamoja na kuwataka CWT kurudi katika meza ya mazungumzo ili
kuruhusu madai ya CWT kushughulikiwa na chombo
kilichopaswa kufanya hivyo kisheria. Maombi hayo yalisikilizwa siku ya
Ijumaa tarehe 27Julai 2012 na pande zote mbili ziliagizwa kukamilisha maelezo
na kuyawasilisha Mahakamani. Serikali ilipangiwa kuwasilisha maelezo yake siku ya Jumatatu
tarehe 30 Julai 2012 saa nne asubuhi na CWT ilipangiwa kuwasilisha maelezo yake
siku ya Jumanne tarehe 31 Julai 2012 saa sita mchana na shauri hilo
litasikilizwa saa saba mchana.
3.0
MAMBO AMBAYO YAMEKUWA YAKIJITOKEZA
Katika kipindi ambapo CWT iliwasilisha
kusudio la mgogoro na hatimaye kusajili Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA),
kumekuwa na ushawishi kutoka katika vikundi mbalimbali kuhamasisha mgomo wa
walimu wote nchi nzima endapo Serikali itashindwa kutimiza matakwa ya CWT. Ushawishi huo umekuwa ukifanyika kwa njia
mbalimbali zikiwemo za ujumbe mfupi wa simu
na kupitia vyombo vya habari.
Aidha, kumekuwa na ujumbe unaopotosha ukweli
unaosambazwa kwenye simu za viganjani na magazeti unaoonesha kuwa kada za
ualimu wanapata viwango vya chini vya mshahara ikilinganishwa na kada za Afya,
Utafiti, Kilimo / Mifugo na Sheria japo wana sifa za kitaaluma zinazofanana. Ujumbe huo una
lengo la kupotosha umma na hususan walimu ili kushawishi kuungwa mkono na
walimu ambao wengi hawana taarifa sahihi kuhusu suala hilo.
4.0 TARATIBU ZA MIGOMO KISHERIA
Sheria
ya Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma Sura 105 Kifungu cha 26 (1) na
(2) kimefafanua utaratibu utakaofuatwa wakati watumishi wa Umma wanapotaka
kufanya migomo / kumfungia nje mwajiri.
Masharti hayo ni;
(i). Kuwepo
na mgogoro au malalamiko,
(ii). Mgogoro
huo uwe umeshindwa kupata suluhu,
(iii). Kura
ya kukubali kufanya mgomo iwe imepigwa na watumishi wengi wa sekta husika chini
ya usimamizi wa Afisa kazi, na
(iv). Notisi
ya siku sitini ya kusudio la kufanya mgomo iwe imewasilishwa Serikalini baada
ya siku ya kura ya nia ya kufanya mgomo.kufanyika.
Mtumishi
yeyote atakayekiuka masharti tajwa hapo juu anaweza kuchukuliwa hatua za
kinidhamu.
Sheria
ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 chini ya Kifungu cha 80 kinatoa
haki na masharti ya kufuata pale mtumishi anapotaka kujiunga na mgomo. Masharti hayo ni;
(i).
Kuwepo na mgogoro wa kimaslahi;
(ii). Mgogoro
uwe umewasilishwa tume ya usuluhishi;
(iii). Mgogoro huo uwe umeshindwa kupata suluhu ndani
ya siku thelathini kwa mujibu wa kifungu cha 86 (4) kikisomwa pamoja na kifungu
cha 87 (1&2);
(iv). Mgomo
uwe umeitishwa na chama cha wafanyakazi na kuungwa mkono na wanachama wengi kwa
mujibu wa katiba ya chama; na
(v). Wafanyakazi
pamoja na chama watoe notisi ya saa 48 ya kusudio la kufanya mgomo kwa mwajiri.
Sheria
zote hizo mbili zimetoa taratibu
zinazotofautiana endapo mtumishi / chama kinapotaka kujihusisha katika mgomo. Kutofautiana kwa taratibu hizo, kumeifanya CWT
kuchagua utaratibu chini ya Sheria ya
Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 ambao mchakato wake ni mfupi zaidi. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 83(4) g cha
Sheria hiyo, mwajiri hatalazimika kulipa mshahara kwa
mtumishi aliyeshiriki katika mgomo kwa kipindi ambacho mtumishi atakuwa kwenye
mgomo.
5.0
ATHARI
ZA MGOMO
Migomo huleta athari mbalimbali katika jamii
husika ikiwemo:
·
Wanafunzi kukosa haki yao ya msingi ya kufundishwa na kujifunza na kusababisha matokeo mabaya ya mitihani; na
·
Uvunjifu wa amani katika sehemu za kazi.
6.0
HITIMISHO
Kwa
vile shauri hili bado lipo Mahakamani, mgomo wa Walimu kwa sasa ni batili. Tumepokea
taarifa za watu kunyanyaswa, kupigwa na kuharibiwa mali zao na mali za Serikali
kunakofanywa na baadhi ya walimu ambao wanataka kuendelea kususia kufundisha.
Jambo
hili si sawa na si busara kwa mtu mwenye taaluma ya ualimu kujihusisha na
vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria na taratibu kwa maslahi yake binafsi.
Tunapenda kuwahakikishia wananchi wote na walimu ambao hawajajihusisha na
vitendo hivi kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vitawalinda na
kuwahakikishia usalama wao.
Lakini
pia tunapenda kuwatahadharisha wote wanaojihusisha na vitendo viovu kama
kuwatisha wenzao, kuwapiga, kuwaharibia mali au kwa njia yoyote kuwanyanyasa
kwa sababu ya kuwa hawajawaunga mkono kugomea kufundisha kuwa, serikali
itachukua hatua kali dhidi yao. Serikali inatoa onyo kwa baadhi ya walimu ambao
wanashawishi na kuwatumia wanafunzi katika mgogoro huu, hii si sawa na sihaki
kabisa. Wanafunzi wasihusishwe wala kutumiwa kwani mgogoro huu ni baina ya
Serikali na walimu.
Mwisho
tunapenda kuwasihi wazazi na walezi kuwa wasikubali, wawazuie na wawakataze
watoto wao kutumiwa au kuhusishwa kwenye mgogoro huu ambao utawahatarishia
usalama na maisha ya watoto wao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment