TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUSITISHWA KWA FAO LA KUJITOA
Irene Isaka, Mkurugenzi wa SSRA |
Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kutoa ufafanuzi juu ya
mafao ya kujitoa. Ufanunuzi huu unakwenda sambamba na taarifa mbalimbali ambazo
zimekuwa zikitolewa na vyombo vya habari na kuleta mkanganyiko miongoni mwa
Wanachama na Wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Kufuatia hali hiyo, Mamlaka
inatoa ufafanuzi ufuatao:
- Marekebisho
kuhusu kusitisha fao la kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya
Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata
mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha uzeeni.
-
Ni kweli kuwa Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii pamoja na Sheria ya Mamlaka zimefanyiwa marekebisho. Mchakato wa
marekebisho hayo ulihusisha wadau kwa kuzingatia utatu yaani wawakilishi kutoka
Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha waajiri pamoja na Serikali.
-
Kwa kutambua tofauti ya ajira, tofauti ya
mazingira ya kazi, tofauti ya sababu za ukomo wa ajira, na umuhimu wa
Mwanachama kunufaika na michango yake wakati angali katika ajira, Mamlaka
inaendelea na mchakato wa kuandaa miongozo na kanuni za mafao ambazo lengo lake
ni kuboresha maslahi ya Wanachama. Miongozo na kanuni hizo zitajadiliwa na
Wadau wakiwemo Wafanyakazi, Waajiri na Serikali kabla ya kuanza kutumika.
-
Kufuatia kuanza
kutumika kwa Sheria hiyo maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha
miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuiwezesha Mamlaka na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau.
-
Tangazo hili
halitowahusu Wanachama waliojitoa kabla ya tarehe 20/07/2012.
- Mamlaka
inakanusha vikali kwamba, sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali
au kwa sababu mifuko imefilisika. Tunapenda kuwahakikishia kwamba Mifuko yote
ipo thabiti na michango yote ya Wanachama ipo salama.
-
Hivyo, Mamlaka
inawaomba Wanachama na Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kuwa na utulivu
wakati mchakato huu ukiendelea kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya
Mwanachama.
Imetolewa na kitengo cha
Mawasiliano na Uhamasishaji
SSRA-Makao Makuu
No comments:
Post a Comment