Friday, July 13, 2012

MWANZA YAZINYANYASA TIMU ZA DAR, YATINGA FAINALI COPA COCA-COLA 2012

Wachezaji wa timu ya Mwanza wakishangilia baada ya kuitoa Kinondoni kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 0-0 na kutinga nusu fainali ya Copa Coca Cola Jumatano. Vijana hao leo wametinga fainali baada ya kuitoa Temeke kwa magoli 3-1. Picha: Sanula Athanas

TIMU ya vijana wa Mwanza imetangulia kwenye fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 baada ya leo asubuhi (Julai 13 mwaka huu) kuilaza Temeke kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
 
Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1. Mwanza walitangulia kufunga dakika ya tatu kupitia kwa Jamal Mtegeta kabla ya Temeke kusawazisha kwa penalti dakika ya 56 iliyowekwa wavuni na Baraka Ntalukundo.
 
Mabao mengine ya Mwanza yaliyoipatia tiketi ya kucheza fainali keshokutwa (Jumapili) yalifunga katika dakika 30 za nyongeza. Mtegeta alitikisa wavu katika dakika ya 94 kabla ya Dickson Ambundo kukwamisha la tatu dakika ya 108.
Mwanza waliingia nusu fainali baada ya kuitoa timu nyingine ya Dar es Salaam ya Kinondoni kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0 Jumatano.
 
Nusu fainali ya pili itachezwa leo jioni ikikutanisha timu za Morogoro ambayo kwenye robo fainali iliibamiza Mara mabao 4-0 na Tanga iliyopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma.
 
 

No comments:

Post a Comment