Mourinho akiwa kibaruani |
MADRID, Hispania
KIFUNGO cha mechi mbili alichopewa
kocha Jose Mourinho wa Real Madrid kwa kosa la kumtia kidole cha machoni kocha
msaidizi wa Barcelona, Tito Vilanova kimeondolewa ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa msamaha wa jumla, Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) lilisema
jana.
Uamuzi huo, uliotangazwa kwenye
mkutano mkuu wa RFEF mjini Madrid, umeibua uwezekano wa kutokea malumbano kati
ya shirikisho hilo na Barca, ambao rais wao Sandro Rosell alisema mwezi
uliopita kwamba kamwe hatakubali vitendo vya ukorofi vya Mourinho kuachwa bila
kutolewa adhabu.
Kocha huyo mtata raia wa Ureno
alifungiwa baada ya kumshambulia Vilanova, ambaye hivi sasa ametwaa mikoba ya
ukocha wa Barca kutoka kwa Pep Guardiola, kwa kumfuata kwa nyuma na kumtia
kidole cha macho wakati wa mechi yao ya mwisho ya kuwania taji la ‘Super Cup’
msimu uliopita.
Kifungo hicho, ambacho kilitolewa kwa
ajili ya Super Cup tu, kiliondolewa na rais wa RFEF, Angel Maria Villar, ambaye
alitumia mamlaka yake kusamehe baadhi ya wachezaji na makocha baada ya kuchaguliwa
tena katika uchaguzi mkuu.
"Vifungo vya hadi mechi nne na vya
mechi mbili kwa uwanja havitatekelezwa," RFEF iliamua, kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa ndani ya mkutano.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa kufungiwa mechi
moja kwa Vilanova kwa kosa la kujibu
mapigo ya Mourinho pia kumefutwa.
Wote sasa wanaweza kuwepo katika
mabenchi ya timu zao wakati Real ambao ni mabingwa wa La Liga na Barca
waliotwaa Kombe la Mfalme watakapokutana mwezi ujao kuwania Super Cup 2012, mechi
mbili za nyumbani na ugenini za kuashiria ufunguzi wa msimu mpya.
Rosell alisema mwezi uliopita kuwa
klabu yake itapinga uamuzi wowote ule wa kumsamehe Mourinho.
"Kama akisamehewa (Mourinho), tutazungumza
na mamlaka husika, hatutaruhusu aachwe bila kuadhibiwa."
No comments:
Post a Comment