Tuesday, July 31, 2012

GAZETI MWANAHALISI WASHANGAA KWANINI SERIKALI HAIKWENDA MAHAKAMANI

Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers inayochapisha gazeti la Mwanahalisi, Saeed Kubenea
Ukurasa wa mbele wa nakala mojawapo ya gazeti lililofungiwa la Mwanahalisi
Uongozi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers inayochapisha gazeti la kila wiki la Mwanahalisi wameelezea kusikitishwa kwao na hatua ya serikali ya kulifungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana na kusema kuwa hatua hiyo inakwenda kinyume na katiba ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Saeed Kubenea, alisema kuwa kufungiwa kwa gazeti hilo pia kunatokana na sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa inakiuka katiba.
  
Mwanasheria wa kampuni hiyo, Dk. Mshana, alishangazwa na hatua ya serikali kukiuka katiba kwa kulifungia gazeti la Mwanahalisi, badala ya kuchukua hatua ya kwenda kuwashitaki mahakamani kama mdai waliyoyatoa ni sahihi.

Jana, serikali ilitangaza kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai kwamba limekuwa likichapisha habari na makala za uchochezi, uzushi na pia zinazokiuka maadili ya uandishi wa habari.

Hatua hiyo ya kulifungia Mwanahalisi imechukuliwa ikiwa ni siku chache tu baada ya gazeti hilo kuchapisha habari zilizowatuhumu baadhi ya maafisa wa usalama wa taifa kuwa ndio waliohusika na tukio la kumteka kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka; ambaye alishambuliwa kikatili na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande na sasa anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, Idara ya Usalama wa Taifa ilikanusha taarifa za kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka na kuziita kuwa ni za ‘uzushi’.  

No comments:

Post a Comment