"Nyororo" la vijana wakisubiri kwenyea kuonyesha "maujuzi" yao mbele ya majaji wa Epiq Bongo Star Search mjini Lindi jana. |
Majaji wa Epiq Bongo Star Search kutoka kushoto, Joachim Kimario a.k.a Master Jay, Ritha Paulsen na Salama Jabir wakifuatilia kwa makini vipaji vya waimbaji wa Lindi jana. |
Na Mwandishi Wetu
IKIWA ni mara ya kwanza kwa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la EBSS kutafuta vipaji katika mkoa wa Lindi, vijana mkoani hapa wameipongeza Epiq Bongo Star Seach kuwafikia mkoani kwao mwaka huu.
Wakizungumza katika ukumbi wa Police Officers Mess mkoani hapa, vijana hao wamesema wanaishukuru EBSS kwa kuwakumbuka kwani vitu vingi huishia mkoani Mtwara.
"Matamasha na mashindano mbalimbali yote huishia Mtwara, sie tumesahaulika, kwakweli tunaishukuru sana EBSS," alisema mmoja wa washiriki, Amani Fabian.
Naye jaji mkuu wa shindano hilo, Ritha Paulsen aliwataka wana-Lindi kujishirikisha katika sanaa ya muziki ili kuitumia vyema sanaa hiyo katika kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo.
Akizungumzia nafasi ya Lindi katika sanaa nchini, Ritha alisema kuwa mbali na mkoa huo kufanya vema katika ngoma za asili pia wanaweza kufanya vema katika nyimbo za kisasa na ndio maana mwaka huu EBSS 2012 imeamua kuufikia mkoa huu.
"Nikiwa kama Jaji Mkuu wa EBSS 2012 ninatambua kuwa kuna vipaji vingi vilivyojificha na ndio maana mwaka huu tukasema kuwa hapana ni lazima tufike mkoa huu na tumeanza kuona vipaji vya kufa mtu," alisema Ritha.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Zantel, Awaichi Mawalla aliwataka vijana hao kutambua nguvu ya muziki katika kuongeza kipato chao cha kila siku na kuhakikisha kuwa wanawekeza katika muziki.
"Lengo letu kama Zantel tunataka kuhakikisha kuwa tunawatengenezeeni vijana fursa ya kujiinua katika maisha kupitia njia mbalimbali kama muziki na vinginevyo, sasa kazi kwenu sisi tunawapa kila fursa vijana mnayoitaka," alisema Awaichi.
Wakati huohuo, vijana waliojitokeza mkoani hapa ni wengi kwa ajili ya kushiriki katika nafasi hii adimu ambayo inahitaji washiriki watano kutoka kila mkoa watakaowakilisha katika ngazi ya taifa.
No comments:
Post a Comment