Moja kati ya 'stori' kubwa zilizoongoza matoleo ya hivi karibuni ya gazeti la Mwanahalisi. |
Sehemu ya ukurasa wa mbele wa toleo la hivi karibuni la gazeti la Mwanahalisi |
Gazeti la kila wiki la Mwanahalisi
limefungiwa kwa muda usiojulikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni
kuandika habari na makala za uchochezi.
Sababu nyingine ya kufungiwa kwa Mwanahalisi imeelezwa kuwa
ni pamoja na habari na makala zake kujenga uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi
kukosa imani na vyombo vya dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano
wa nchi.
Akisoma tamko la serikali leo jijini Dar es salaam, Kaimu
Mkurugenzi Wizara ya Habari (MAELEZO), Phabian Lugaikamu, alisema kuwa matoleo
ya Mwanahalisi, namba 302, 303 na 304 ya mwaka 2012 na mengine yaliyotangulia,
yalichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
Aidha alisema kuwa mhariri huyo mara zote katika utetezi
wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha katiba ya nchi kinachotoa uhuru wa
kutoa maoni na kwa makusudi kutokunukuu kifungu ca 30 cha katiba hiyo
kinachoweka ukomo wa uhuru.
"Serikali imeamua kulifungia gazeti hilo kutochapishwa kwa
muda usiojulika kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba
25(i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa tangazo la
serikali namba 258 lililochapishwa katika gazeti la Serikali na kutolewa jijini
Dra es salaam Julai 27,2012," alisema.
ALIYEMTEKA DK. ULIMBOKA
Uamuzi huu wa kulifungia Mwanahalisi umekuja ikiwa ni siku
chache tu baada ya gazeti hilo
kuwatuhumu na kuwataja kwa majina baadhi ya maafisa wa Idara ya Usalama wa
Taifa kuwa ndio waliohusika na tukio la kumteka kiongozi wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kwa habari iliyokuwa na kichwa cha habari
kinachosema: "Aliyeteka Ulimboka huyu hapa".
Hivi karibuni, gazeti hilo pia lilichapisha taarifa
zilizowahusisha watu wa Usalama wa Taifa kwa habari iliyokuwa na kichwa
kisemacho:"Njama za mauaji zafichuka"
Hata hivyo, Idara ya Usalama wa Taifa ilitoa taarifa za kukanusha
kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka na kuwataka wananchi wapuuze tuhuma hizo
dhidi yao kwani ni za 'uzushi'.
Hii si mara ya kwanza kwa gazeti la Mwanahalisi kufungiwa.
Mara ya mwisho, lilifungiwa kwa miezi mitatu kutokana na tuhuma zinazofanana na
zile zinazotolewa sasa.
No comments:
Post a Comment