Thiago Silva (kusho) na Zlatan Ibrahimovic |
KOCHA wa PSG, Carlo Ancelotti anatarajia kuwakaribisha nyota wawili wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva klabuni kwake wiki ijayo.
Ofa ya PSG ya euro milioni 65 imekubaliwa na Milan kwa ajili ya kuwasajili nyota hao.
"Tunawatarajia watue PSG," alisema Ancelotti. "Natumai watakuja hapa mapema, lakini sitasema kingine chochote kuhusu wachezaji hawa wawili, ambao ni bora kabisa duniani.
"Kila mtu anajua kwamba tunawahitaji Ibrahimovic na Silva. Tunafanya juhudi kukamilisha usajili wao na kuna uwezekano watakuwa wachezaji wa PSG mapema sana, bado haijawa rasmi."
Jana, rais wa AC Milan, Silvio Berlusconi alitangaza kuwauza Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva kwa PSG.
Berlusconi aliwathibitishia waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri nje ya makao makuu ya klabu hiyo kwamba dili la euro milioni 65 limeafikiwa.
"Ndio, nimewauza Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva kwa PSG," Berlusconi alisema.
"Tutaokoa paundi milioni 150 katika miaka miwili," aliongeza waziri Mkuu huyo wa zamani wa Italia, akimaanisha mishahara ya wachezaji hao.
No comments:
Post a Comment