Friday, July 13, 2012

ADEBAYOR HATIMAYE ATUA RASMI TOTTENHAM

Adebayor

Emmanuel Adebayor wa Tottenham Hotspur akishangilia goli lake pamoja na wachezaji wenzake Kyle Walker na Aaron Lennon wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa White Hart Lane jijini London, England Mei 13, 2012.

TOTTENHAM Hotspur wameafiki ada ya uhamisho ambayo haitajwi kwa ajili ya kumsajili straika wa Manchester City, Emmanuel Adebayor.

Na Man City sasa huenda wakawa tayari kutuma maombi yao rasmi ya kutaka kumsajili straika wa Arsenal, Robin van Persie, mara nyota huyo wa Togo atakapokamilisha uhamisho.

Adebayor (28) alifunga magoli 18 katika mechi 37 alizoichezea Spurs kwa mkopo msimu uliopita.

Straika huyo atakuwa mchezaji wa tatu kutua Tottenham katika kipindi hiki cha usajili baada ya kusajiliwa kwa beki wa Ajax, Jan Vertonghen na Gylfi Sigurdsson.

Inafahamika kwamba Man City wamedhamiria kupunguza mzigo wa mishahara wanayolipa kabla ya kuingia sokoni kusaka nyota wapya. Adebayor ameripotiwa kuwa mmoja wachezaji wanalipwa fedha nyingi zaidi katika klabu hiyo wakati Wayne Bridge ameondoka tayari kujiunga na Brighton.

Mapema mwezi huu Van Persie (28), alitangaza kwamba hataongeza mkataba wake Arsenal. Huku mkataba wa straika huyo ukiwa unamalizika mwisho wa msimu, Arsenal wanakabiliwa na hatari ya kumpoteza bure kama hawatamuuza kabla ya Januari 31.

Inafahamika kwamba pamoja na Man City, Manchester United na Juventus pia zinamhitaji straika huyo ambaye, alifunga magoli 41 katika mechi 53 kwa klabu yake na timu ya taifa msimu uliopita.

Adebayor mwenyewe alihamia Manchester City akitokea Arsenal, akisaini kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 25 Julai 2009, akifunga magoli 15 katika mechi 34.

Baada ya kupoteza nafasi yake kwa kocha Roberto Mancini, alijiunga kwa mkopo na Real Madrid ya La Liga Januari 2011, lakini waliamua kutompa mkataba wa kudumu.

Aliisaidia Spurs kumaliza katika nafasi ya nne katika Ligi kuu ya England msimu uliopita na wiki hii kocha mpya wa Tottenham, Andre Villas-Boas alisema: "Tunafuraha sana kwamba tuko na Adebayor katika jahazi moja."

Adebayor alifunga magoli 46 katika mechi 105 alizochezea Arsenal baada ya Arsene Wenger kumnunua kutoka Monaco January 2006.

No comments:

Post a Comment