STARS WATUA, KOCHA KIM ATAKA MECHI ZA KUJIPIMA
Na Mwandishi Maalumu
TIMU ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imewasili Jijini Dar es Salaam Jumanne usiku ikitokea nchini Msumbiji ambako iliondolewa katika michuano ya kufuzu kucheza mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.
Mara baada ya kuwasili, kocha Kim Poulsen amekisifia kikosi chake na kusema licha ya kuondolewa katika mashindano hayo na The Mambas ya Msumbiji kwa penalti 6-7, wachezaji wake walijiuma hadi dakika ya mwisho na kusawazisha goli moja walilokuwa wamefungwa.
“Vijana walicheza vizuri na tumeona mabadiliko makubwa ikilinganishwa na mechi chache ambazo tumecheza tangu tutangaze kikosi hiki kipya,” alisema Poulsen.
Aliiomba TFF ifanye juhudi za kuhakikisha Stars, ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inapata nafasi ya kucheza mechi nyingi za kirafiki ili kujiandaa na michuano ijayo.
“Kikosi hiki kina vijana wengi na wanahitaji kupata uzoefu hivyo ni vizuri tukipata mechi nyingi za kirafiki ili tujiandae vizuri na michuano ijayo,” alisema.
Poulsen alisema ana imani na kikosi chake na kwamba amewataka wachezaji wakiongeza juhudi.
Akiwa nchini Msumbiji, Poulsen alitoa wito kwa wchezaji wa Stars wajitume katika klabu zao ili wapate nafasi nyingi za kucheza ambazo zitawapa uwezo mkubwa wakiwa katika timu ya taifa.
Kwa sasa kambi ya timu ya taifa imevunjwa hadi mwezi Agosti ambapo wachezji wanatarajiwa kuitwa kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na timu ambayo watapangiwa na TFF.
Taifa Stars kwa sasa inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia Bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager.
No comments:
Post a Comment