CHINA WAJIANDAA KUMPOKEA DROGBA
Drogba akiwa na kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya |
SHANGHAI, China
WAKATI wachezaji wa Shanghai Shenhua wakijiandaa
kucheza na mchezaji mwenzao mpya, Didier Drogba, kocha wao Sergio Batista alisema
anakaribia kumnasa mchezaji mwingine wa kimataifa wa Colombia, Giovanni Moreno
ili kuipa nguvu timu yao inayohaha katika ‘Chinese Super League’, Ligi Kuu ya
China.
Drogba ambaye ni mshambuliaji wa
timu ya taifa ya Ivory Coast, alitangaza kwamba amekubali kusaini mkataba wa
kuichezea Shanghai kwa miaka miwili na nusu juzi, lakini badala ya kuridhika na
usajili huo, Batista ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina ameendelea
kufukuzia mchezaji mwingine mwenye jina kubwa.
Moreno ( 25), ambaye hivi sasa
anaichezea klabu ya Racing ya Argentina, ametajwa kuwa ni mchezaji sahihi wa
kumsaidia Drogba na Batista alisema kuwa anatarajia kiungo huyo mshambuliaji
atatua China kabla ya mwisho wa mwezi.
"Pengine bado kuna vikwazo
kutoka katika klabu ya Moreno. Natarajia kwamba atatua Shanghai wiki hii au
wiki ijayo," kocha huyo aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa
kila wiki wa klabu yake na waandishi wa habari jana.
Shanghai walisema kwamba ndoto
yao imekuwa kweli wakati wakithibitisha kumsajili Drogba na kwamba mshambuliaji
huyo anaweza kushirikiana katika kushambulia na mchezaji wa zamani wa timu ya
taifa ya Ufaransa, Nicolas Anelka.
Drogba ataungana na wenzake Julai
baada ya mkataba wake na Chelsea kumalizika na Batista ana shauku kubwa ya kuwa
na mshambuliaji huyo mwenye nguvu, anayefahamika pia nchini China kwa jina la 'The
Beast'.
KUPANDA KIWANGO
Wakati uhamisho wa Drogba, ulioripotiwa
kuambatana na masharti ya mshahara wa dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni
500) kwa wiki ukiwa gumzo duniani, baadhi ya mashabiki nchini China wamekerwa
kuona kwamba fedha nyingi zinalipwa kwa mchezaji mmoja tu na sio kuwekezwa
katika kuwaendeleza vijana kwa ajili ya timu ya taifa.
Hata hivyo, beki wa Shanghai, Dai
Lin anaamini kwamba kuwasili kwa Drogba kunaweza kuwasaidia katika kukuza
viwango vyao.
"Uhamisho wa Drogba ni mzuri
kwa timu yetu na kwa soka la China," Dai aliwaambia waandishi wa habari.
"Tuna mengi ya kujifunza kwa
nyota wa kimataifa kama yeye, ikiwa ni pamoja na weledi na ujuzi wa soka. Na
zaidi ya yote, Drogba ni mchezaji ambaye ameshatwaa taji la Ligi ya Klabu
Bingwa Ulaya."
Wachezaji wa Shanghai na
mashabiki wao watakuwa na matumaini kwamba Drogba, aliyefunga penati
iliyoisaidia Chelsea kuifunga Bayern Munich na kutwaa ubingwa wa Ulaya mwezi
uliopita, anaweza kuibeba mara moja baada ya timu hiyo kuanza msimu vibaya.
Shanghai wanakamata nafasi ya 12
katika msimamo wa ligi wenye timu 16 ikiwa ni baada ya kuanza vibaya katika
mechi 13. Batista ni kocha wao wa tatu msimu huu baada ya kuwatimua mchezaji wa
zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Jean Tigana na kusitisha kipindi kifupi cha
uongozi wa muda wa Anelka, licha ya kusudio la mshambuliaji huyo kutaka
kuendelea na kibarua hicho.
"Kila mmoja
katika timu yetu amefurahi sana kwa sababu tumekuwa tukitarajia tangazo hili
kwa muda mrefu," alisema kiungo wa Shanghai, Yu Tao.
No comments:
Post a Comment