Wee mkali, ila acha mapepe.... kocha Mancini (kulia) akimpa nasaha Balotelli katika mechi mojawapo ya klabu yao ya Manchester City |
MILAN, Italia
KOCHA wa Manchester City, Roberto Mancini amemwagia sifa Mario
Balotelli baada ya kuonyesha kiwango cha juu na kufunga mabao yote yaliyoipa timu
ya taifa ya Italia ushindi wa mabao 2-1 katika nusu fainali yao ya Euro 2012 dhidi
ya Ujerumani juzi Alhamisi.
Siku zote Balotelli amekuwa akichukuliwa kuwa ni mchezaji mtukutu kwa sababu
ya tabia yake ya kujiingiza kirahisi katika migogoro isiyokuwa na msingi ndani na nje ya uwanja. Hata
hivyo, Mancini, ambaye alimfundisha wakati
akiwa Inter Milan na baadaye akamsajili Man City, hajawahi kumkatia tamaa mshambuliaji
huyo mwenye miaka 21 na ameendelea kuamini kwamba ipo siku ataimarika kifikra
na kutambua kipaji chake.
"Kwakweli amenifurahisha," kocha huyo Muitalia aliliambia
Gazzetta dello Sport.
" Ni wakati ambao anaweza kuupita na kubadilika kutoka
kuwa mchezaji mzuri na kuwa mchezaji nyota.
"Na dhidi ya Hispania katika fainali Jumapili, natumaini
kwamba ataibeba timu. Wakati wake wa kujijengea heshima umewadia."
Mancini alisema vilevile kwamba alijua mapema kuwa Balotelli angefunga
mabao mawili dhidi ya Ujerumani, ingawa hakufurahishwa na kitendo cha mshambuliaji
huyo cha kujipa kadi ya njano kizembe kufuatia shangilia yake ya kuvua baada ya
kupachika goli ‘kali’ la pili.
"Ilionekana wazi kwamba Mario angefunga mabao mawili; nilijua
tu," mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia alisema.
"Nilijua kuwa ule
ulikuwa ni usiku wake na kwamba ndiye ambaye angeleta tofauti ya mechi.
"Nilifikiria nini baada ya goli lake la pili? Ni kwamba
angeweza kufunga bao jingine. Lakini ni aibu kwamba alivua jezi. Asingeruhusu
kulimwa kadi ya njano."
Italia sasa watakabiliana na Hispania katika mechi itakayochezwa
mjini Kiev kesho na kumpata bingwa wa Euro 2012, mechi ikitarajiwa kupigwa
kesho Jumapili kuanzia saa 3:45 (kwa saa za Afrika Mashariki)
No comments:
Post a Comment