Thursday, June 28, 2012

KOCHA WA TAIFA UHOLANZI VAN MARWIJK AJIUZULU


Bert van Marwijk

ROTTERDAM, Uholanzi
BERT van Marwijk amejiuzulu nafasi yake ya ukocha wa timu ya taifa ya Uholanzi juzi baada ya kuamua kwamba hawezi kuendelea kuifundisha timu hiyo kufuatia kutolewa kwa aibu katika Euro 2012, chama cha soka cha Uholanzi (KNVB) kimesema.


"Nilikuwa na shaka, lakini mwisho nimeamua kwamba napaswa kuchukua hatua hii," Van Marwijk, ambaye mwaka jana aliongeza mkataba wake kwa miaka minne hadi 2016, alisema katika taarifa kwenye tovuti ya KNVB (www.knvb.nl).


Uholanzi waliofika fainali ya Kombe la Dunia 2010, walitolewa kwenye Euro 2012 kwa kufungwa mechi zote za tatu za hatua ya makundi, ikiwa ni kiwango chao kibovu kabisa katika michuano mikubwa.


Kipigo cha 1-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Denmark kilifuatiwa na vipigo viwili vilivyofanana vya 2-1 kutoka kwa Ujerumani na Ureno.


Vyombo vya habari vya Uholanzi vimemtuhumu Van Marjwik kwa kushindwa kwa timu hiyo, wakimshutumu kwa ubishi, lakini wachezaji wengi wamemsapoti. "


"Van Marwijk alifanya kazi nzuri sana kutuongoza kufika fainali ya Kombe la Dunia 2010 na kushika nafasi ya kwanza katika viwango vya FIFA," alisema mkurugenzi wa KNVB, Bert van Oostveen.


"Inauma kwamba tunalazimika kusema kwaheri hivi sasa lakini ni lazima tuwe wa kweli."


Van Marwijk, 60, alichukua madaraka ya kuifundisha timu ya taifa Julai 2008 baada ya Marco van Basten kujiuzulu. Chini ya uongozi wake, Uholanzi ilishinda mechi 14 za kimashindano mfululizo kabla ya kulala 1-0 dhidi ya Hispania katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010.


Wadachi pia walionyesha kiwango cha juu katika mechi ya kuwania kufuzu kwa Euro 2012, wakishinda mechi tisa mfululizo kabla ya kufungwa na Sweden katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu.

No comments:

Post a Comment