Monday, June 25, 2012
ITALIA YAITOA ENGLAND, YAISUBIRI UJERUMANI
KIEV, Ukraine
ALESSANDRO Diamanti alifunga penalti iliyowapeleka Waitalia waliostahili katika nusu fainali ya Euro 2012 kwa kuibwaga England kwa "matuta" 4-2 baada ya dakika 120 kumalizika bila ya goli katika mechi ambayo Waingereza walitumia usiku mzima wa jana "kusaka mpira kwa tochi".
Diamanti alifunga penalti hiyo baada ya Ashley Young na Ashley Cole kukosa penalti zao kwa upande wa England na kuipeleka Italia katika nusu fainali ambapo sasa itacheza dhidi ya Ujerumani mjini Warsaw, Poland Alhamisi.
Italia ilitawala sehemu kubwa ya mechi hiyo ya kwanza michuano ya mwaka huu kufikia hatua ya muda wa nyongeza, wakifanya majaribio zaidi ya 30 ya kufunga langoni mwa England. Daniele De Rossi, aliyefumua shuti la umbali wa mita 25 katika dakika ya tatu, na Diamanti wote waligongesha nguzo za lango la England.
Riccardo Montolivo, mara mbili, na Mario Balotelli, mara nyingi, pia walikaribia kufunga wakati Antonio Nocerino alifunga goli katika dakika ya 114 ambalo lilikataliwa kwa kuwa alikuwa ameotea wakati safu ya ulinzi ya England 'ikichanwa' mfululizo baada ya kuanza vyema na hata wenyewe kukaribia kupitia kwa Glen Johnson na Wayne Rooney.
Waliofunga penalti kwa upande wa Italia walikuwa Mario Balotelli, Andrea Pirlo, Antonio Nocerino na Diamanti wakati Riccardo Montolivo alipiga nje. Waliofunga penalti kwa upande wa England walikuwa Steven Gerrard na Wayne Rooney wakati Young aligongesha 'besela' na ya Cole ikidakwa na kipa Gianluigi Buffon.
Mechi ya nusu fainali ya kwanza itakuwa baina ya Ureno na Hispania keshokutwa Jumatano mjini Donetsk, Ukraine wakati kesho yake Alhamisi Ujerumani watawavaa Italia mjini Warsaw
Fainali itapigwa Jumapili mjini Kiev, Ukraine.
KIEV, Takwimu za mechi ya robo fainali ya Euro 2012 baina ya Italia na England iliyoamuliwa kwa kupigiana penalti baada ya kumalizika kwa sare ya bila magoli kwenye Uwanja wa Olympic jana usiku:
England Italia
1. Magoli yaliyofungwa 0 0
2. Jumla ya mashuti 9 35
3. Mashuti yaliyolenga lango 4 20
4. Kona 3 7
5. Kuotea 1 2
6. Faulo 15 11
7. Kadi za njano 0 2
8. Kadi nyekundu 0 0
9. Kumiliki mpira 36% 64%
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment