Wednesday, June 27, 2012

GRAND MALT YADHAMINI TAMASHA LA FILAMU TANGA

Muandaaji wa tamasha la filamu la TOFF,  Musa Kissoky (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Wengine pichani ni Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butala (kushoto) na nyota wa Bongo Muvies, Vincent Kigosi a.k.a Ray. Picha: Interllectuals Communications LTD
KINYWAJI cha Grand Malt leo kimetangaza kuendelea kudhamini tamasha maarufu la filamu hapa Tanzania lijulikanalo kama Tanzania Open Film Festival (TOFF) ambalo hufanyika jijini Tanga kila mwaka.

Akizungumza katika uzinduzi wa tamasha la mwaka huu, meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam alisema; "Kinywaji cha Grand Malt ndio mdhamini mkuu wa Tamasha la Filamu Tanzania. Tamasha hili limekuwa likifanyika katika Jiji la Tanga na limeonyesha kupendwa sana na wakazi wa Jiji la Tanga.

"Kwa mwaka huu wa 2012, tamasha hili linaanza Juni 30 hadi Julai 6. Kwa kipindi chote hiki, Grand Malt imejipanga kuhakikisha kuwa tunafanya uhamasishaji wa kutosha katika jiji la Tanga, ili kuwawezesha wakazi wa Tanga na maeneo ya jirani kuweza kuhudhuria tamasha hili. Tunawakaribisha watu wote wenye mapenzi na filamu zetu za Kitanzania kufika na kushuhudia tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi."

Naye Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema: "Kama mtakumbuka, mwaka jana Grand Malt iliamua kushirikiana na Kampuni ya Sophia Records, ambao ndio waandaaji na waasisi wa tamasha hili. Ushirikiano wetu ulikuwa mzuri, kwani tulijifunza mambo mengi kuhusu tamasha hili, lakini kikubwa zaidi tulijionea jinsi wananchi wanavyozipenda filamu za Kitanzania maarufu kama “Bongo Movies” na jinsi walivyo na kiu ya kuwaona wasanii wa Bongo Movies ana kwa ana.

"Kufuatia umuhimu huo, hatua ya kwanza tuliyochukua ni kusaini mkataba wa udhamini wa miaka mitatu na kampuni ya Sophia Records, na hatua nyingine itakuwa kuweka utaratibu wa kulipeleka tamasha hili katika mikoa mingine ya Tanzania na hatimaye kuliweka katika hadhi ya kimataifa. Grand Malt inawaahidi wakazi wa Tanga na Watanzania wote kwa ujumla, kuwa tamasha hili litakuwa na mvuto wa aina yake na hatimae kutumika kulitangaza taifa letu kupitia tasnia hii ya filamu ambayo kwa sasa inakua kwa kasi kubwa."

Mkurugenzi wa Sophia Records, waandaaji na waasisi wa tamasha hili, Musa Kissoky alisema: "Kwanza kabisa tunatoa shukurani za dhati kwa Grand Malt kwa kukubali kushirikiana nasi katika kuboresha na kuendeleza tamasha hili. Sophia Records iliona kiu ya Watanzania kupata fursa ya kuona filamu za wasanii wetu hasa katika jukwaa kubwa la wazi, lakini pia kukutana na wasanii wenyewe na kubadilisha na nao mawazo juu ya tasnia hii, hivyo tukaanzisha tamasha hili ambalo sasa linajulikana kama Grand Malt Tanzania Open Film Festival. Tunawashukuru sana wasanii wa Bongo Movies, hususan uongozi wao, kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia katika kuhakikisha mafanikio ya matamasha haya."

Akizungumzia maandalizi ya tamasha la mwaka huu linaloanza Jumamosi, Kissoky alisema; "Maandalizi yote yapo tayari, kama ilivyo kawaida, tamasha litafanyika katika viwanja vya Tangamano na litakuwa likianza asubuhi hadi usiku. Tumeandaa burudani nyingi zitakazosindikiza maonyesho haya ya filamu kwa siku zote saba, na hakutakuwa na kiingilio, hivyo watu wote wanakaribishwa kuja kujionea filamu zetu na kukutana na wasanii waliobobea katika tasnia hii ili wabadilishane mawazo."



No comments:

Post a Comment