Wednesday, June 27, 2012

BALE ASAINI MIAKA MINNE SPURS


LONDON, England
KIUNGO Gareth Bale amesaini mkataba wa miaka minne na klabu yake ya Tottenham Hotspur ambao utamweka White Hart Lane hadi mwaka 2016, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England ilisema jana.

"Nimekuwa hapa kwa miaka mitano sasa na nimefurahia kila dakika," Bale aliiambia tovuti ya Tottenham (www.tottenhamhotspur.com).

"Mashabiki wamekuwa wema kwangu na ningependa kurejesha fadhila zao kwa kufanya makubwa kwa klabu yangu. Klabu inakua na nataka kuwa sehemu ya jambo hilo, hivyo imekuwa vyema kwamba dili limekamilika," aliongeza nyota huyo wa timu ya taifa ya Wales ambaye amekuwa akihusishwa na mipango ya kutua Barcelona.

"Naipenda klabu na mashabiki na nataka kutoa mchango wangu katika kuturidisha katika Ligi ya Klabu Bingwa - ambako ndiko tunakostahili," alisema.

Tottenham bado hawana kocha kufuatia kufukuzwa kwa Harry Redknapp mapema mwezi huu.

Spurs walikuwa wa nne msimu uliopita lakini wamekosa nafasi ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa kwa sababu Chelsea walitwaa ubingwa wa mashindano hayo ya Ulaya huku wakiwa wamemaliza wa sita katika msimamo.

No comments:

Post a Comment