Jaji Mkuu wa Epiq Bongo Star Search, Ritha Paulsen |
Na Mwandishi Wetu
JAJI Mkuu wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search (EBSS) 2012, Ritha Paulsen amewataka wakazi wa mkoa wa Lindi wenye uwezo wa kuimba kujitokeza kwa wingi kesho katika ukumbi wa Police Officers Mess ili kupata nafasi ya kuwakilisha mkoa huo kwenye shindano hilo.
Ritha aliyekuwa akizungumzia usaili wa EBSS 2012 kwa mkoa wa Lindi alisema kuwa anatambua kuwa mkoa wa Lindi una vijana wengi na wenye vipaji vya kuimba, na ndio maana kwa mara ya kwanza mwaka huu EBSS itaufikia mkoa huo.
"Tangu shindano hilo lianze miaka sita iliyopita, mwaka huu ndio tumelifikisha mkoa wa Lindi, ili kuhakikisha tunapata vipaji kutoka karibu kila kona ya nchi hii," alisisitiza Ritha.
Shindano hilo lilianzia mkoa wa Dodoma halafu likaelekea visiwani Zanzibar ambako kote walipata wawakilishi watano watano wenye vipaji vikubwa ambavyo alisema ana hakika vitaleta ushindani mkubwa mwaka huu.
"Mimi binafsi nimeshangazwa na uwezo wa hawa vijana wa kuimba na kumiliki eneo la kuimbia na nashindwa kuelewa walikuwa wapi muda wote huu, yani nikisema kuwa EBSS mwaka huu ni moto inaamisha kuwa itakuwa na ushindani mkubwa kweli kweli," alisema Ritha.
Alisema kwa kuwa mwaka huu EBSS inatoa fursa kwa washiriki wa umri kuanzia miaka 16, bado wanaangalia vipaji vya washiriki katika umri huo kwa kuwa bado hawajawapata.
Shindano hilo mwaka huu linadhaminiwa na kampuni ya huduma za simu za mikononi ya Zantel, ambao watatoa Sh. milioni 50 kwa mshindi na mkataba wa kurekodi.
No comments:
Post a Comment