Del Bosque |
DONETSK, Ukraine
HISPANIA walisaidiwa na bahati kutinga
fainali ya tatu mfululizo ya michuano mikubwa na Ureno ndio waliocheza vizuri
katika muda mwingi wa mechi, alisema kocha Vicente del Bosque wa Hispania baada
ya kushinda kwa penati 4-2 katika nusu fainali yao ya Euro 2012.
Mahasimu hao hawakufungana katika
dakika 90 za kawaida na pia katika muda wa ziada uliowafanya wamalize mechi
hiyo kwa dakika 120, lakini walionyesha soka safi na lenye ushindani mkali
katika muda wote.
Matokeo ya penati yalitegemea ni timu
gani yenye bahati zaidi ambapo mwishowe mabingwa wa Dunia na Ulaya waliibuka
kidedea.
Wakati Hispania wakiongoza kwa penati
3-2, Bruno Alves wa Ureno alishuhudia penati yake ikirudi uwanjani baada ya
kugonga ‘besela’ huku ya Cesc Fabregas iliyogonga pia mlingoti wa goli ikijaa
wavuni na kuwapa ushindi Hispania.
"Tulikuwa na bahati sana wakati
wa upigaji wa penati," Del Bosque aliuambia mkutano na waandishi wa
habari.
"Lakini napenda kutoa pongezi
zangu kwa timu ya Ureno kwa sababu walionyesha soka zuri, lakini sisi tulikuwa
na bahati, kwakweli safari hii tulikuwa na bahati sana."
Alisema vilevile kuwa kwa ujumla,
Ureno walicheza vizuri zaidi, wakijilinda vizuri mara kadhaa kuliko Hispania na
kuonekana hatari wakati wakishambulia, lakini wachezaji aliowaingiza, Jesus Navas na Pedro badala ya David Silva na
Xavi, walibadili kila kitu.
"Tulitengeneza nafasi nyingi za
kufunga wakati walipoingia, tuliwashambulia zaidi na ilikuwa muhimu kuwaingiza.
Tulionekana kuchoka na hivyo tulihitaji kasi ya ziada, hasa katika dakika za
nyongeza wakati Pedro alipoingia," alisema.
Del Bosque alisema kuwa hakupata ugumu
wowote kuchagua wachezaji wa kupiga penati kwani Xabi Alonso (aliyekosa),
Andres Iniesta, Gerard Pique, Sergio Ramos na Fabregas wote ni wapigaji makini.
"Hakukuwa na tatizo, Cesc
aliniambia kwamba anataka kupiga penati ya mwisho itakayotupa ushindi na ndivyo
alivyofanya," aliongeza.
Kwa ushindi huo, Hispania watacheza
fainali ya Euro 2012 itakayofanyika Jumapili dhidi ya mshindi wa nusu fainali
nyingine kati ya Italia na Ujerumani.
No comments:
Post a Comment