Friday, February 8, 2013

SIMBA YAENDA KUJIWINDA KWA OLJORO


Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 9 mwaka huu) kwa mechi nne ambapo Oljoro JKT itaikaribisha Simba jijini Arusha.

Mechi hiyo namba 129 itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid huku Simba ikiingia na kumbukumbu ya sare katika mechi yake iliyopita dhidi ya JKT Ruvu wakati wenyeji wao wakiwa wameshinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 tu utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Kagera Sugar na Mgambo Shooting. Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Amon Paul kutoka Musoma mkoani Mara.

Toto Africans baada ya kufanya vibaya katika mechi tatu zilizopita ugenini imerejea nyumbaji jijini Mwanza itakapoumana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo utaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na African Lyon ambayo imepata huduma za kocha mpya Salum Bausi kutoka Zanzibar. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Bausi kuiongoza timu katika VPL.

Maofisa wengine wa mechi hiyo ni mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Rashid, mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani wakati mwamuzi wa mezani ni John Kanyenye wa Mbeya. Kamishna wa mechi hiyo ni Rashid Rwena kutoka Ruvuma.

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele kwa siku moja ambapo sasa itafanyika Jumapili (Februari 10 mwaka huu) katika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment