Monday, February 25, 2013

WAZIRI WA MICHEZO AIFUTA KATIBA YA TFF ILIYOTUMIWA NA KINA MTIGINJOLA KUWAFYEKA KINA MALINZI, WAMBURA... AAMURU ITUMIKE KATIBA YA 2006...ATNGAZA PIA KUMPIGA CHINI MSAJILI WA VYAMA KWA KUIPITISHA KIHOLELA KATIBA YA SASA YA TFF!

Katiba hii si halali...! Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mkangara (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo wakati akitangaza kuifuta katiba ya sasa ya TFF na kulia ni naibu wake, Amos Makalla.  
Rais wa TFF, Leodeger Tenga


Serikali imeingilia kati sakata la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.

Serikali pia imetangaza kumtema msajili wa vyama vya michezo nchini, David M. Rwezahula kutokana na kupitisha katiba hiyo yenye kasoro kinyume cha sheria na taratibu zilizopo za Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema kuwa serikali imefikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa taratibu za kurekebisha katiba za vyama vya michezo kwa mujibu wa sheria za BMT zilizotungwa na Bunge zimekiukwa katika usajili wa katiba ya TFF.

Amesema Sheria Na. 12 ya BMT na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 1971 na kanuni za usajili za baraza hilo Na. 442 za mwaka 1999 hazikufuatwa wakati wa usajili wa katiba hiyo yenye kurasa 56 iliyosaniwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga.

“Kanuni ya BMT Na. 11(1) inayoelezwa wazi utaratibu wa marekebisho ya katiba, haikufuatwa. Kimsingi TFF walitakiwa wajaze fomu Na. 6,7,8 na 9 kwa mujibu wa kanuni za BMT. Wakishajaza fomu baada ya siku 14, msajili anatakiwa kuwajibu. Kama anakataa, anatumia fomu Na. 10 au fomu Na. 11 kama anakubali. TFF hawakufiuata taratiobu hizi. Nalisema hili kwa sababu suala la katiba si jambo dogo,” amesema Dk. Fenella.

Waziri huyo akitumia mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya 13(1) ya sheria za BMT, alitaka kufutwa matumizi ya katiba ya TFF iliyopitishwa kwa njia ya waraka Desemba 15, 2012 na kuagiza itumike katiba ya 2006 katika shughuli zote za shirikisho hilo kwa sasa hadi pale kamati ya utendaji ya TFF itakapoitisha mkutano mkuu ambao utapitisha marekebisho ya katiba hiyo kwa kufuata kanuni za BMT.

“Ifahamike kwamba hakuna chama chochote cha michezo nchini kilicho juu ya BMT. Kwa kuwa zipo taarifa kuwa FIFA watakuja Tanzania, msajili na TFF wawataarifu FIFA kuhusu maelekezo haya ya kutumia katiba ya mwaka 2006 na wawaambie hali halisi iliyojitokeza,” amesema.

Dk. Fenella alisema vilevile kuwa atateua msajili mwingine kuchukua nafasi ya Rwezahula ikiwa ni sehemu ya hatua za kinidhamu alizopanga kuzichukua dhidi ya watendaji wote wa wizara yake waliohusika na upitishwaji wa katiba hiyo.

Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.

Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee.


Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili kufuatilia kinachotokea nchini.

Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa  ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment