Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jana walifanya maandamano makubwa jijini Dar
es Salaam hadi katika Makao Makuu ya
Polisi na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
wakililalamikia Jeshi hilo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya
wizi na kulawitiwa wanavyofanyiwa na genge la watu katika hosteli iliyoko
Kigamboni.
Mamia ya wanafunzi hao walianza kuandamana
kutoka chuoni kwao katikati ya Jiji saa
4:40 asubuhi na kuwasili makao makuu ya Jeshi hilo ambayo yapo pia makao Makuu
ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi saa 5:33 asubuhi.
Baada ya kuwasili, walisema dhumuni la
maandamano yao ni kutaka kuonana na Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema au Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ili kufikisha kilio chao kwao.
Rais wa Serikali
ya Wanafunzi wa IFM, Michael Charles, alisema wanafunzi wamekuwa wakivamiwa na
kuibiwa mali zao ikiwamo kompyuta ndogo (laptop), kubakwa na kulawitiwa katika
hosteli ya Kigamboni wilayani Temeke.
Charles alisema licha ya matukio hayo kuripotiwa katika kituo cha polisi Machava kilichopo
Kigamboni, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi na
hivyo kuwafanya wanafunzi wahisi kuwa huenda vitendo hivyo vina baraka za
polisi.
“Juzi tulivamiwa
na wenzetu wawili wakapigwa mapanga, tukaibiwa kompyuta na wenzetu wengine
wakalawitiwa, ndiyo maana tumeamua kuandamana kupeleka malalamiko yetu kwa
sababu tumeona kinachofuata tunaweza
kuuawa,” alisema Charles.
Charles alisema
mpaka sasa idadi ya komputa za wanafunzi zilizoibwa ni 300 ambazo zimekuwa
zikiibwa kila siku.
Awali
baadhi ya wanafunzi walizuiliwa eneo la jengo la PPF wasifike Makao
Makuu ya Jeshi la Polisi.
Hata hivyo,
wanafunzi hao walikwama kuonana na IGP Mwema na Dk. Nchimbi baada ya kuzuiliwa
na maafisa wa jeshi hilo katika lango kuu la kuingilia badala yake na walielezwa
na askari waliokuwa langoni hapo kuwa wachague watu watatu ili waruhusiwe
kwenda kuonana na viongozi hao.
Jitihada zilizofanywa na maafisa wa polisi H. Mbezi na N. Marijan, kuwataka
wachague wenzao watatu kwenda kutoa malalamiko yao ziligonga mwamba kufuatia
baadhi ya wanafunzi hao kudai kwa wanaovyoifahamu polisi, wale watakaokwenda huko watawekwa chini ya ulinzi na
suala lao halitasikilizwa tena.
Baadaye wanafunzi hao walibadilisha maelezo kwa
kudai kuwa wanataka kuonana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, ili wamweleze kilio chao.
Ilipofika saa 6:03 mchana, Kova aliwasili Makao
Makuu ya Jeshi la Polisi na kuzua shangwe kubwa kutoka kwa wanfunzi hao ambao
walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu kwamba huyo ndiye atakayeweza kuwasikiliza
kilio chao na kukipatia ufumbuzi.
Kova baadaye alizungumza na wanafunzi hao kwa
kuwataka afuatane nao hadi Kigamboni ili watuhumiwa wa vitendo hivyo wakamatwe
haraka.
Msafara wa Kova ambaye alikuwa katika gari namba
PT 1574 pamoja na Charles na Waziri Mkuu wa IFM aitwaye Mangesho, ulianza
safari ya kuelekea Kigamboni saa 6:11 mchana, huku ukifuatana na mamia ya wanafunzi
wa chuo hicho.
Hata hivyo, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya idadi kubwa ya wanafunzi hao kutaka
kuvuka katika kivuko eneo la Ferry na hivyo kuulazimu uongozi wa kivuko hicho
kusimamisha safari ili kupunguza wengine.
Halikuwa jambo rahisi kuwapunguza wanafunzi
hao katika kivuko na hivyo kusababisha mabishano yaliyochukua muda mrefu kati ya uongozi wa kivuko, Jeshi la Polisi
likiongozwa na Kova pamoja na wanafunzi hao ambao walikuwa wanagoma kupunguzwa.
Mabishano hayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu hadi walipokubaliana kusafirishwa
kwa awamu.
"Kitaalamu hatuwezi kuondoa kivuko kwa sababu
idadi ya watu ni kubwa na hilo haliruhusiwi, labda wengine wapunguzwe,”
alisema Mhandisi wa Mambo ya Bahari, Reuben Materu.
Kwa upande wake, Kova alisema: “ Hili jambo
halihitaji ushabiki. Ni la kiutaalamu zaidi, tunaweza kuwaruhusu wavushwe hivyo
hivyo, lakini ikaleta madhara mengine makubwa zaidi.”
Mabishano hayo yalizuia safari za abiria
wengine hadi wanafunzi wote waliposafirishwa kwa awamu.
POLISI WAFYATUA
MABOMU
Licha ya
wanafunzi kukubaliana na Polisi kuelekea katika Uwanja wa Machava, lakini
baadhi ya wanafunzi walidaiwa kukiuka makubaliano
hayo baadaye na kuelekea kituo cha
polisi cha Kigamboni huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kulaani Jeshi la Polisi na kuona hivyo, askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakafyatua
mabomu ya machozi kwa takribani dakika 20.
Mbali na kufyatua mabomu, pia waliwakamata
wanafunzi zaidi ya 100 na kuwapeleka katika kituo cha polisi Kigamboni, lakini
baadaye waliachiwa na kuelekea sehemu ya uwanja kwa ajili ya mazungumzo na
Kova.
Baadhi ya wananchi wa Kigamboni walijitokeza kutoa ushuhuda,
akiwamo kijana mmoja aliyesema:
“Ni kweli wanafunzi huwa wanaibiwa. Ninawafahamu hao wezi na kama mkitaka nitawapeleka.”
Symphorasa Ndyamukama, mkazi wa Kigamboni na
mmoja wa wamiliki wa hosteli za wanafuzni hao, alisema alishawahi kutoa taarifa
hizo za uhalifu polisi, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Kova ambaye alikuwa
amefuatana na Kamanda wa Polisi wa mkoa
wa Temeke, Englibert Kiondo, alimtaka atoe ufafanuzi juu ya taarifa hizo.
Kamanda Kiondo alijibu kwamba taarifa hizo za
uhalifu hazijawahi kuripotiwa polisi rasmi isipokuwa walikuwa wanazisikia tu.
Kutokana
na hali hiyo, Kamanda Kova alimuagiza Kiondo kulifanyia kazi mara moja suala hilo ili kubaini wahalifu na kuwakamata.
Alisema vilevile kuwa atamteua askari atakayeshirikiana
naye katika kuwabaini wahalifu katika eneo hilo, na kuagiza zoezi hilo kuanza
jana mara moja.
No comments:
Post a Comment