Monday, January 7, 2013

RODGERS ATETEA GOLI LA "MKONO WA SUAREZ"

Straika wa Liverpool, Luis Suarez akimiliki mpira kwa mkono kabla ya kufunga goli la ushindi dhidi ya timu ya "mchangani" ya Mansfield Town wakati wa mechi yao raundi ya tatu ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa One Call mjini Mansfield, England jana Jumapili Januari 6, 2013. Liverpool walishinda 2-1.

Straika wa Liverpool, Luis Suarez akimpita kipa wa timu ya "mchangani" ya Mansfield Town,Alan Marriott, wakati wa mechi yao raundi ya tatu ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa One Call mjini Mansfield, England jana Jumapili Januari 6, 2013. Liverpool walishinda 2-1.
Straika wa Liverpool, Luis Suarez akimuacha kipa wa timu ya "mchangani" ya Mansfield Town, Alan Marriott, baada ya kumiliki mpira kwa mkono wakati wa mechi yao raundi ya tatu ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa One Call mjini Mansfield, England jana Jumapili Januari 6, 2013. Liverpool walishinda 2-1.

Straika wa Liverpool, Luis Suarez akishangilia goli lake dhidi ya timu ya "mchangani" ya Mansfield Town wakati wa mechi yao raundi ya tatu ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa One Call mjini Mansfield, England jana Januari 6, 2013. Liverpool walishinda 2-1.

KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers anaamini kwamba waamuzi ndiyo waliopaswa kulaumiwa, siyo Luis Suarez, baada ya straika huyo wa kimataifa wa Uruguay kutumia mkono kumpiga chenga kipa kabla ya kufunga goli la ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ya "mchangani" ya Mansfield Town katika mechi yao ya raundi ya tatu ya Kombe la FA.

Liverpool walipata goli la kuongoza la mapema dhidi ya wapinzani wao hao wa "mchangani" kupitia kwa mshambuliaji wao mpya Daniel Sturridge, kabla ya Suarez kutumia mkono wake kumpiga chenga kipa kisha kuutumbukiza mpira wavuni.

Suarez pia alitumia mikono kuokoa goli lililoinyima Ghana nafasi ya kuwa timu ya kwanza Afrika kutinga nusufainali Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini 2010.

Hata hivyo, Rodgers hakutaka kumshutumu straika wake wake nyota, ambaye aliwachefua zaidi mashabiki wa timu mwenyeji kwa kushangilia goli hilo akionyeshea mkono wake.

"Nimeliangalia tena na hakuna shaka kwamba kwamba alishika," Rodgers aliiambia ESPN. "Nadhani refa na waamuzi wengine walichokuwa wakiangalia ni kwamba hakushika kwa makusudi, jambo ambalo halikuwa makusudi.

"Nilizungumza na mwamuzi wa akiba baada ya goli kuhesabiwa na kumuuliza kama alishika, kwa sababu mimi sikuweza kuona, na alisema ni kweli alishika. Hivyo ni wazi kwamba ni bahati mbaya kwa Mansfield na bahati kwetu kwamba tumepewa goli.

"Haitokei sana kwenye soka, nikiwa muwazi.

"Hutarajii itokee na si kazi ya Luis kuamua. Alienda pale, hakushika kwa makusudi - mpira ulidunda ukamgusa mkononi.

"Hilo ni suala la refa kuamua. Ndiyo maana wanalipwa kwa kazi hiyo na ndiyo maana wao ni waamuzi weledi.

"Andre Marriner, nadhani, alichezesha vyema leo na waamuzi wenzake. Ni moja ya mambo yale machache aliyokosea."

No comments:

Post a Comment