RUFAA YANGU KATIKA TUHUMA ZA EPA NA MWIGULU NCHEMBA
|
Mhe. John Mnyika |
|
Mhe. Mwigulu Nchemba |
|
Mhe. Jenista Mhagama |
Na John Mnyika
Nimekata Rufaa dhidi ya uamuzi wa Mwenyekiti Mhagama
suala la EPA; nasubiria Spika aitishe kamati ya kanuni ili bunge liendeshwe kwa
ufanisi:
Katika kipindi cha takribani wiki mbili nimeulizwa kwa
nyakati mbalimbali na wananchi kwenye mitandao ya kijamii na wanahabari kwa
njia ya simu kutaka kufahamu iwapo nilitimiza azma ya kukata rufaa juu ya
uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge Jenister Mhagama kutoa muongozo wa kunitaka
kuwasilisha ushahidi katika suala alilolisema yeye mwenyewe badala ya kunipa
fursa ya kueleza tuhuma nilizonazo dhidi ya Mwigulu Nchemba na hatimaye
kuwasilisha ushahidi juu ya tuhuma hizo.
Kwa kuwa swali na suala hilo limekuwa likirudiwarudiwa
kwenye mijadala mbalimbali bila taarifa sahihi kutolewa, naomba kutoa majibu
kwamba tayari nilishawasilisha malalamiko kwa mujibu wa Kanuni ya 5(4) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge toka tarehe 12 Julai 2012 dhidi ya uamuzi huo wa
Mwenyekiti wa Bunge ambao haukuzingatia matakwa ya Kanuni za kudumu na
uendeshaji bora wa Bunge.
Ninachosubiria sasa ni Spika kuitisha kikao cha kamati
ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na
kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Nimekata rufaa kwa sababu tatu: mosi; mwenyekiti
amenitaka kuwasilisha ushahidi wa suala ambalo sikulisema mimi bali amelisema
yeye; pili, Sikupewa nafasi ya kueleza tuhuma nilizotaka kueleza dhidi ya
Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na badala yake Mwenyekiti aliendelea kunitaka
nizungumzie tuhuma alizozieleza yeye; mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala
ambalo nililiombea kuhusu utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a) juu ya
madai ya Mwigulu Lameck Nchemba juu ya hotuba ya kambi rasmi ya upinzani ya
Ofisi ya Rais.
Katika barua yangu kwa katibu wa Bunge nilieleza pia
kuwa ni muhimu kamati ya kanuni ikakutana kabla ya kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kushughulikia uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai
tarehe 12 Julai 2012 katika kikao cha ishirini na mbili cha mkutano wa nane
kwamba “Kamati hiyo sasa ndiyo itashughulikia ushahidi huo na kuthibitisha
kwamba Mheshimiwa Mwigulu naye kumbe alikuwa anahusika na wizi wa fedha
za EPA”, ili kamati hiyo isifanye uamuzi kwa kurejea muongozo usiokuwa sahihi.
Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi
ya Bunge (Hansard) za kikao cha kumi na tano cha tarehe 3 Julai 2012 cha
mkutano wa nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Bunge
Jenister Mhagama alisema na kufanya maamuzi kwamba: “Mheshimiwa Mnyika,
umesema kwamba unao ushahidi, naomba unisikilize kusudi utakaponijibu ujibu
mwongozo nitakaokupa kwa mujibu wa taratibu. Mheshimiwa Mnyika umesema hapa na
kulithibitishia Bunge, waheshimiwa wabunge naomba tusikilizane. Umesema unao
ushahidi na umelithibitishia Bunge kwamba yeye Mheshimiwa Lameck Mwigulu
Nchemba ni mmoja wa watuhumiwa katika kesi hizo za EPA. Sasa na mimi nakupa
siku saba ulete ndani ya Bunge tuhuma zinazomgusa Mheshimiwa Mwigulu.”
Katika rufaa yangu nimeeleza kutoridhika dhidi
ya muongozo huo wa Mwenyekiti wa Bunge na kwa kutumia kanuni ya 5 (4)
nimewasilisha sababu za kutoridhika na uamuzi huo kama ifuatavyo:
Sababu ya Kwanza; Mwenyekiti amenitaka kuwasilisha ushahidi wa suala
ambalo sikulisema mimi bali amelisema yeye:
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge sikutamka
maneno kwamba ninao ushahidi wa kulithibitishia bunge kwamba Lameck Mwigulu
Nchemba ni mmoja wa watuhumiwa wa kesi hizo za EPA kama ambavyo amedai
Mwenyekiti wa Bunge kama nilivyomnukuu hapo juu.
Nilichokisema, na nanukuu:
“Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nasimama kwa kanuni ya 64 (1) (a) hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina
ukweli, Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza ili aelewe kwamba
anachokisema anakitambua; alikuwa mtumishi wa Benki Kuu ambayo ilikumbwa na
kashfa ya ufisadi wa EPA na sasa ni Mweka Hazina wa Chama cha CCM inayotuhumiwa
kwenye wizi wa pesa za KAGODA... lakini usalama wa taifa hatujawahi kusikia
popote katika kuzuia. Usalama wa Taifa kuhusika kwenye kuzuia. Kwenye Bunge
hili, kambi ya upinzani ilileta ushahidi wa Barua ya usalama wa Taifa kwenye
kashfa hiyo ya EPA ambayo anaifahamu vizuri . Usalama wa taifa ukizuia jambo
lisije bungeni kujadiliwa badala ya kuibua ufisadi, kuzuia ufisadi usitokee,
ushahidi huo uko ndani ya kumbukumbu za Bunge na ukitaka nilete ushahidi wa
namna gani matukio ya uhalifu na hili ni lalamiko ndani ya idara ya usalama wa
taifa ya watumishi wa usalama wa taifa wanatoa ushirikiano ,wanatoa taarifa
viongozi wa juu yao hawazishughulikii taarifa na katika hotuba ya
ofisi ya rais haijatuonyesha popote idara ya usalama wa taifa ilipozuia matukio
ya uhalifu kwenye hotuba hii tunayozungumza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo
naomba mchangiaji atambue huo ukweli na aache propaganda na aache siasa kwa
sababu yeye ni mmoja wa watuhumiwa”
Sababu ya Pili; Sikupewa nafasi ya kueleza tuhuma nilizotaka kueleza
dhidi ya Mwigulu Lameck Nchemba na badala yake Mwenyekiti aliendelea kunitaka
nizungumzie tuhuma alizozieleza yeye.
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard)
niliposema “aache propaganda na aache siasa kwa sababu yeye ni mmoja wa
watuhumiwa”, Mwenyekiti aliingilia kati kabla ya mimi kueleza kuwa yeye ni
mmoja wa watuhumiwa wa nini na kuelekeza ifuatavyo:
“Mheshimiwa Mnyika, naomba uthibitishe
hilo kwamba na yeye ni mmoja wa watuhumiwa kabla sijatoa mwongozo na kama unao
uthibitisho kwamba na yeye ni mmoja wa watuhumiwa naomba utoe uthibitisho huo
kama huna ufute kauli yako ili niweze kufanya maamuzi ya kinachofuata ili tuendelee
na kazi za kuwawakilisha wananchi. Mheshimiwa Mnyika una uthibitisho wa kwamba
Mheshimiwa Mwigulu ni mmoja kati ya wanaotuhumiwa?”
Nilipoanza tu kueleza kuwa:“Mheshimiwa
Mwenyekiti, alikuwa mmoja wa watumishi wa Benki Kuu...” kabla hata ya
kuendelea kueleza ni mtuhumiwa wa nini katika taasisi ambazo nilitaka yeye
alizitumikia au anaendelea kuzitumikia Mwenyekiti akanikatisha na kudai
yafuatayo “Mheshimiwa Mnyika umesema hapa na kulithibitishia (bunge)”.
Ilibidi niingilie kati na kuomba tena
haki ya kueleza ni Mwigulu Lameck Nchemba ni mmoja kati ya wanaotuhumiwa na
nini kwa kumuomba Mwenyekiti anipe haki ya kujieleza na kueleza tuhuma kama
ifuatavyo:
“Niambie kwanza niseme tuhuma gani
ninazo dhidi yake na nitoe ushahidi wa hizo tuhuma. Nimesema ni mmoja wa
watuhumiwa. Niruhusiwe niseme anazotuhuma gani na nitoe ushahidi wa hizo
tuhuma.”
Hata hivyo Mwenyekiti alikataa kunipa nafasi ya
kueleza tuhuma nilizotaka kueleza dhidi ya Mwigulu Lameck Nchemba na badala
yake Mwenyekiti akafanya uamuzi wa kunitaka nilete ushahidi wa tuhuma
alizozieleza yeye.
Sababu ya Tatu; Mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala ambalo nililiombea kuhusu
utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a) juu ya madai ya Mwigulu Lameck
Nchemba juu ya hotuba ya kambi rasmi ya upinzani ya Ofisi ya Rais:
Nilitaka utaratibu ili aweze kuondoa maneno potofu
aliyoyatoa huu ya nukuu juu ya ukweli ambao kambi rasmi ya upinzani iliueleza
kwamba “…. Usalama wa Taifa hatujawahi kusikia popote wamehusika katika kuzuia
mchakato huo japokuwa wanakuwa na taarifa za kutosha.”
Hata hivyo, Mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala
hilo ambalo nilitangulia mimi kuliomba badala yake akaishia kunitaka kuleta
ushahidi wa tuhuma alizozieleza yeye mwenyewe mwenyekiti bila kufanyia kazi
utaratibu ambao niliomba uzingatiwe. Hali ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa
ulikuwa ni upendeleo kwa Mwenyekiti hakumkatisha Nchemba alipotoa tuhuma dhidi
ya kambi rasmi ya upinzani kumtaka athibitishe alipotajwa tu ni mmoja wa
watuhumiwa bila tuhuma hizo kuelezwa Mwenyekiti alitoa muongozo wa tuhuma
alizozisikia yeye na kutaka ushahidi uletwe kwa tuhuma hizo.
Pamoja na kuwawakilisha wananchi katika masuala
mengine ya maendeleo bungeni, hatua hii ya kukata rufaa inalenga kudumisha
ukweli na kuhakikisha kwamba bunge linaendeshwa kwa kuzingatia kanuni bila
upendeleo ili kuweza kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisimamia serikali kwa
ufanisi zaidi.
Wako katika kuwawakilisha wananchi,
John
Mnyika (Mb)