Wabunge nchini wanaenzi sana amani. Licha ya tofauti zao
za mara kwa mara bungeni na ambazo wakati mwingine huongozwa zaidi na
ushabiki wa vyama vyao kiasi cha kuzomeana na hata kushtakiana mbele ya
Spika wa Bunge. bado waheshimiwa hao huonekana kuwa ni kama marafiki
wawapo nje ya 'mjengo' wa Bunge.
Hali hiyo ilijidhihirisha jana wakati Mhe. Tundu Lissu, Mbunge wa Jimbo
la Singida Mashariki (CHADEMA) alipoonekana nje ya 'mjengo' akichati
bila hofu na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro (CCM), Mhe. Christopher Ole
Sendeka.
Ikumbukwe kuwa juzi, Mhe. Tundu Lissu alimlipua Ole Sendeka wakati
akizungumza na waandishi wa habari, akimtaja kuwa naye ni miongoni mwa
wabunge wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kutanguliza maslahi yao binafsi na
kutumiwa kuwatetea wafanyabiashara wa mafuta walionyimwa tenda ya
kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.
Kutokana na Lissu kumtaja Ole Sendeka juzi, Mbunge huyo wa Simanjiro
alikuja juu na jana akaomba mwongozo wa Spika ili ajue kama ibara ya 100
inayotoa kinga kwa wabunge inaweza kumkwaza katika kutimiza dhamira
yake ya kumburuza Tundu Lissu mahakamani kutokana na kile alichodai kuwa
ni kumdhalilisha kwa kumzushia mbele ya waandishi wa habari kuwa
anatumiwa kuwatetea wafanyabiashara wa mafuta.
Hata hivyo, wakati akitoa ufafanuzi juu ya mwongozo alioomba Ole
Sendeka, Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda, alisema kuwa anampeleka
Tundu Lissu katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili awe
shahidi namba moja kuthibitisha tuhuma kwamba kuna wabunge wanaokula
rushwa na kutumiwa na wafanyabiashara na pia wengine hutetea maslahi yao
binafsi kwa kufanya biashara na TANESCO.
Spika alisema vilevile kuwa ibara ya 100 inamkinga Lissu dhidi ya
kusudio la kuburuzwa mahakamani kwa vile alizungumza na waandishi wakati
akiwa kwenye eneo la Bunge. Akawasihi wabunge kuwa na subira wakati
kamati ya uongozi ikishughulikia tuhuma za kashfa ya rushwa dhidi ya
baadhi ya wabunge, hasa wa kamati aliyoivunja ya Nishati na Madini.
Licha ya mgongano wao wa ndani ya Bunge, waheshimiwa Ole Sendeka na
Tundu Lissu walionekana nje ya Bunge baadaye wakizungumza pamoja pasi na
kuonyesha dalili zozote za uhasama baina yao. Yaani ilikuwa ni amani,
hakuna shari.
Je, wabunge wa nchi nyingine kama Kenya wanaweza? Safi sana!
No comments:
Post a Comment