SAN JUAN, Puerto Rico
MASHINE inayoshikilia maisha ya Hector "Macho" Camacho itaondolewa, mama wa bondia huyo bingwa wa dunia wa zamani ambaye alipigwa risasi ya shavuni, alisema jana, akiashirikia kwamba atawaambia leo Jumamosi madaktari waitoe mashine. Hata hivyo, hayo ni maamuzi ambayo yanapingwa na mtoto mkubwa wa bondia huyo.
Mama wa bondia hiyo, Maria Matias, aliwaambia waandishi wa habari nje ya hospitali ambayo Camacho amelala akiwa hajitambui tangu alipopigwa risasi ya uso kwamba ameamua madaktari waitoe mashine inayosaidia maisha yake, lakini jambo hilo lifanyike baada ya kuwasili Puerto Rico kwa watoto watatu wa bondia huyo leo Jumamosi na kupata nafasi ya kumuona baba yao kwa mara ya mwisho.
"Nilimpoteza mwanangu (Camacho) siku tatu zilizopita. Hivi sasa yuko hai kwa sababu ya mashine tu," mama Matias alisema. "Mwanangu hayuko hai. Mwanangu yuko hai kwa ajili ya watu wanaompenda tu," aliongeza.
Watoto wengine watatu wa bondia huyo walitarajiwa kuwasili wakitokea Marekani usiku wa jana. "Hatutaichomoa mashine, mpaka watakapowasili," mama Matias alisema.
Mkutano mwingine na waandishi wa habari umepangwa kufanywa asubuhi ya leo katika hospitali ya Centro Medico.
Mama wa bingwa huyo wa zamani ndiye mwenye kauli ya mwisho kwenye suala hilo, lakini mtoto wa kwanza wa bondia huyo, Hector Jr., alisema anataka kumuacha baba yake akiwa hai.
"Baba atapambana mpaka mwisho. Baba yangu ni bondia," mtoto huyo wa kiume alisema.
Madaktari wamesema ubongo wa Camacho umeshakufa kutokana na risasi alizopigwa Jumanne usiku katika mji wa nyumbani kwao wa Bayamon. Lakini ndugu na marafiki waliliambia shirika la habari la Associated Press bado wanapambana kama waondoe mashine hiyo ama waiache.
"Ni maamuzi magumu sana, maamuzi mazito sana," bondia wa zamani wa kulipwa Victor "Luvi" Callejas, rafiki wa muda mrefu wa Camacho, alisema katika mahojiano ya njia ya simu. "Jambo la mwisho kabisa ni kukataa tamaa na kupoteza matumaini. Kama hatujakata tamaa na tunayo matumaini, kwanini tusisubiri japo kidogo?"
Aida Camacho, mmoja wa shangazi za bondia huyo, alisema katika mahojiano kwamba familia ingeamua Ijumaa usiku kuhusu kuchangia viungo vilivyopungua.
Wakati ndugu na marafiki wakiendelea kusali kuomba miujiza, rambirambi zimeendelea kuwasilishwa kwenye familia ya Camacho na maandalizi ya msiba na mazishi yameanza.
Gavana Luis Fortuno ameita kuwa hilo ni pigo kubwa la ghafla. "'Macho' daima atakumbukwa kwa uanamichezo wake na upendo ndani na nje ya ulingo," alisema.
Mwingine aliyetuma salamu za rambirambi ni gavana aliyechaguliwa Alejandro Garcia Padilla, ambaye alimshinda Fortuno katika uchaguzi wa Novemba.
"Maisha ya Macho Camacho, kama ya magwiji wetu wengine wa michezo, yaliiunganisha nchi yetu," alisema. "Tulisherehekea mataji yake mitaani na tulimpigia makofi."
Camacho alipigwa risasi akiwa amekaa kwenye gari na rafikie, Adrian Mojica Moreno (49), ambaye aliuawa katika shambulio hilo. Msemaji wa Polisi, Alex Diaz alisema maofisa walikuta vipakti vidogo tisa ya cocaine katika mfuko wa rafikiye na kimfuko cha 10 kikiwa kimefunguliwa ndani ya gari.
Polisi waliripoti kuwa hakuna mtu aliyekamatwa na kwamba wapelelezi wanaendelea kuwahoji mashuhuda. Kapteni Rafael Rosa aliwaambia waandishi wa habari jana Ijumaa kuwa wanafuatilia dondoo kadhaa walizopata, lakini aliongeza kwamba mashuhuda wachache sana wametoa ushirikiano. Alikataa kusema kama Polisi imebaini watuhumiwa fulani.
Hector Camacho Jr. alisema matukio ya uhalifu yanayoiandama Puerto Rico, kisiwa cha Marekani chenye takriban watu milioni 4, yaliripotiwa kuwa 1,117 mwaka jana idadi ambayo ni rekodi.
"Vifo, jela, dawa za kulevya, mauaji," alisema. "Hivyo ndivyo ilivyo mitaa yetu hivi sasa."
Dada za Camacho walisema kuwa wangependa kuusafirisha mwili wa Camacho hadi New York na kwenda kumzika kule. Camacho alikulia mjini Harlem, na akapata jina la utani la "Harlem Heckler."
Alishinda mataji ya ubingwa wa dunia katika uzani wa super lightweight, lightweight na junior welterweight katika miaka ya 1980 na alipigana mapambano makubwa kama dhidi ya Felix Trinidad, Julio Cesar Chavez na Sugar Ray Leonard. Camacho alimpiga kwa KO Leonard mwaka 1997, na kuhitimisha ndoto za kurejea kwa bingwa huyo wa zamani. Camacho alikuwa na rekodi ya 79-6-3.
Camacho alipambana na matatizo mengi binafsi kama utumiaji wa dawa za kulevya, pombe na matatizo mengine maishani mwake. Alihukumiwa kifungo miaka 7 gerezani mwaka 2007 kutokana na kesi ya wizi, lakini jaji aliamua kukifanya kuwa kifungo cha nje na kuacha mwaka mmoja tu gerezani. Aliishia kutumikia wiki mbili gerezani, baada ya kukiuka masharti ya kifungo cha nje. Mkewe pia mara mbili alifungua mashitaka ya kupigwa kabla ya hawajatalikiana.
No comments:
Post a Comment