Monday, November 19, 2012

ROONEY, VAN PERSIE WAACHWA SAFARI YA GALATASARAY

Mashine ya kufungia magoli... Robin van Magoli anapumzishwa
Torres akitolewa kwa kadi ya pili ya njano na refa Mark Cluttenburg dhidi ya Man U


LONDON, Uingereza
MANCHESTER United, ambayo tayari imefuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, itawapumzisha wakali wake kadhaa katika mechi yao ya leo ya Kundi H dhidi ya Galatasaray mjini Istanbul, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imesema leo.

Wayne Rooney, Rio Ferdinand, Ryan Giggs, Paul Scholes, David De Gea na Robin van Persie wote watabaki mjini Manchester, klabu hiyo ilisema katika tovuti yake (www.manutd.com) leo.

Kikosi cha kocha Alex Ferguson kinajumuisha wachezaji saba ambao hawajawahi kucheza michuano hiyo.
Man U, ambayo imeshinda mechi nne, imetinga hatua ya 16-Bora huku wakiwa wamebaki na mechi mbili.

Mabingwa watetezi Chelsea wanahitaji kuonyesha ungangari ambao uliwapa mafanikio msimu uliopita, badala ya "uchovu" walioonyesha kwenye Ligi Kuu ya England, kama wanataka kutinga hatua ya 16-Bora Ulaya kesho.

Pamoja na Man U, Porto na timu iliyoonyesha kiwango cha juu ya Malaga ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ndizo timu pekee ambazo kimahesabu zimefuzu hatua ya mtoano, ingawa timu zitakazosonga mbele zitajulikana zaidi wiki hii.

UEFA inatumia utaratibu mgumu wa kuamua timu ya kusonga mbele na siyo utaratibu wa "tofauti ya magoli" uliozoeleka. Baina ya timu zitakazokuwa zimelingana pointi, kitakachoangaliwa ni timu gani imepata pointi nyingi ilipowakabili waliolingana naye, jambo linalomaanisha kwamba timu zitahitaji kusubiri hadi siku ya mwisho kujua aliyesonga mbele.

Lakini katika uhalisia, Arsenal, Barcelona, Bayern Munich, Celtic, Borussia Dortmund, AC Milan, Paris St Germain, Real Madrid, Schalke 04, Shakhtar Donetsk na Valencia zote zinaweza kusonga mbele kama zitashinda wiki hii.

Chelsea itasonga mbele kesho kama itashinda mechi yao ya Kundi E dhidi ya Juventus mjini Turin, na kutinga hatua hiyo ya 16-Bora kwa msimu wa 10 mfululizo.

Lakini kikosi cha Roberto Di Matteo kinasafiri bila ya ushindi katika mechi nne za Ligi Kuu ya England huku wakitokea katika kipigo kisichotarajiwa cha 2-1 ugenini dhidi ya West Bromwich Albion Jumamosi pale makosa ya ulinzi yalipowagharimu.

"Kwa sababu zisizojulikana Novemba unaonekana mwezi mbaya kwa klabu hii," Di Matteo aliwaambia waandishi wa habari.

Kiwango cha chini cha Fernando Torres hatimaye kimegeuka kaa la moto kwa Di Matteo wiki chache tu baada ya Muitalia huyo kuonekana kila analofanya linakwenda sawa.

Viungo watatu Eden Hazard, Oscar na Juan Mata wameonekana kuvutia macho ya wengi lakini Torres anaonekana kuhaha kuthibitisha thamani yake ya paundi milioni 50.

Hata hivyo, kipigo cha 3-2 nyumbani dhidi ya Manchester United mwishoni mwa Oktoba, ambapo Torres alitolewa kwa kadi nyekundu kwa kujiangusha, na nahodha John Terry kufungiwa mechi nne kwa ubaguzi wa rangi na pia kupata majeraha ya goti vimechangia kuanguka kwa timu hiyo.

Kipigo katika mechi ya leo Italia kitaweka njiapanda matumaini yao ya kutinga 16-Bora na Di Matteo huenda akajaribu kucheza mfumo wa kujilinda zaidi kesho, jambo linalohatarisha nafasi ya Torres.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool amefunga goli moja tu katika mechi saba zilizopita Chelsea na Di Matteo amedokeza kwamba Mhispania huyo huenda akaachwa benchi dhidi ya Juventus kesho.

No comments:

Post a Comment