Friday, November 23, 2012

OBI MIKEL AGEUZIWA KIBAO KESI YA UBAGUZI DHIDI YA REFA MARK CLATTENBURG

Refa Mark Clattenburg (kulia) akizungumza na Obi Mikel wa Chelsea wakati wa mechi dhidi ya Man United.

CHAMA cha Umoja wa Marefa kimeitaka Chelsea amuombe radhi refa Mark Clattenburg na kimlipe fidia baada ya kufutiwa mashitaka ya kutoa maneno ya kibaguzi.

Chelsea walidai kuwa Clattenburg, 37, alitumia lugha "isiyo ya kiungwana" dhidi ya kiungo John Obi Mikel.

Chama cha soka cha England (FA) sasa kimemuona refa huyo hana hatia na Chelsea imekubali maamuzi hayo.

Mwenyekiti wa chama cha marefa, Alan Leighton ametaka refa huyo aombwe msamaha na alipwe hasara ya kipato, fidia ya heshima na mgandamizo wa mawazo alioupata Clattenburg.

Leighton pia ameitaka Chelsea kuchangia "kitita" katika kampeni za kupambana na ubaguzi kama Onyesha Kadi Nyekundu kwa Ubaguzi na Kick It Out.

Katika kuafiki maamuzi ya FA, taarifa ya Chelsea ilisomeka kwamba klabu "imeafiki maamuzi ya Chama cha Soka kuhusu Mark Clattenburg na inapokea suala kwamba FA inatambua kuwa klabu na  wachezaji walikuwa sahihi kuripoti jambo hilo."

Hata hivyo, Chelsea haikuomba radhi moja kwa moja kwa refa huyo.

Ushahidi wa tuhuma za Chelsea ulitoka kwa kiungo Ramires, ambaye, wakati akihojiwa, alifafanua kwamba alisema anahitaji kupata uthibitisho kutoka kwa Mikel kuhusu nini alichokisema Clattenburg.

Mikel, 25, ambaye alikuwa akizungumza na Clattenburg wakati wa tukio, alikuwa jirani zaidi na refa kuliko Ramires lakini hakusikia kile kilichodaiwa kusemwa.

No comments:

Post a Comment