Wednesday, November 21, 2012
HAYA NI MAISHA YA KAWAIDA CHELSEA
Orodha ya makocha NANE walioifundisha Chelsea wakati wa utawala wa mmiliki bilionea wa Urusi Roman Abramovich, baada ya Roberto Di Matteo kutimuliwa leo.
CLAUDIO RANIERI (Septemba 2000-Mei 2004)
Alikuwa madarakani wakati Abramovich alipoinunua klabu hiyo 2003, na Muitalia huyo alishuhudia kuinuka kwa kipaji cha nahodha John Terry na pia aliwanunua wakali wa sasa wa Chelsea, Petr Cech na Frank Lampard. Aliiongoza Chelsea kumaliza ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya England na kuipeleka hadi nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika msimu wake wa mwisho, lakini bado alifukuzwa.
JOSE MOURINHO (Juni 2004-Septemba 2007)
Mtu aliyeweka misingi ya Chelsea mpya, kocha Mreno "msema ovyo" Mourinho aliingia Stamford Bridge baada ya kuiongoza Porto kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na akatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England katika misimu yake miwili ya kwanza. Pia akashinda Kombe la FA Cup na mataji mawili ya Kombe la Ligi, lakini kushindwa kupata mafanikio Ulaya kulimuangusha na akaonyeshwa mlango wa kutokea baada ya kutofautiana na Abramovich katika msimu wake wa nne.
AVRAM GRANT (Septemba 2007-Mei 2008)
Kocha Muisraeli ambaye alikuwa "hajulikani", Avram Grant awali alijiunga na Chelsea kama mkurugenzi wa michezo lakini akapewa kiti hicho cha moto cha ukocha baada ya Mourinho kutimuliwa. Akivuka matarajio, aliiongoza Chelsea kutinga fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mjini Moscow lakini aliishuhudia timu yake ikifungwa kwa "matuta" na Manchester United na akatimuliwa.
LUIZ FELIPE SCOLARI (Julai 2008-Februari 2009)
Kocha mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Brazil, 'Big Phil' Scolari alikuwa na mwanzo mzuri sana Stamford Bridge lakini alitimuliwa miezi saba tu baadaye kufuatia mfululizo wa matokeo ya kufadhaisha. Baadaye alidai kwamba alikuwa akidharauliwa na wachezaji wakongwe katika chumba cha kuvalia.
GUUS HIDDINK (Februari 2009-Mei 2009)
Akiingia madarakani kama kocha wa muda, Hiddink alikuwa na mafanikio licha ya kufanya kazi hiyo sambamba na ajira yake ya kudumu ya ukocha wa timu ya taifa ya Urusi. Mholanzi huo aliiongoza Chelsea kutwaa ubingwa wa Kombe la FA dhidi ya Everton katika mechi ya fainali na alipoteza mechi moja tu katika ya mechi 22 alizoiongoza timu hiyo lakini hakushawishiwa kubaki.
CARLO ANCELOTTI (Juni 2009-Mei 2011)
Muitalia mwenye rekodi nzuri, akiwa ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na AC Milan, aliingia kwa kishindo Chelsea na aliiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Ligi na Kombe la FA katika msimu wake wa kwanza. Hata hivyo, Chelsea ilitolewa katika robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliofuata na akaripotiwa kufukuzwa kwenye ngazi za uwanja wa Goodison Park baada ya kulala 1-0 ugenini dhidi ya Everton.
ANDRE VILLAS-BOAS (Juni 2011-Machi 2012)
Villas-Boas alikuwa msaidizi wa Mourinho klabuni Porto na aliwasili Stamford Bridge akiwa na sifa kubwa baada ya kuiongoza klabu hiyo ya Ureno kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya Ureno, Kombe la 'FA' la Ureno na Ligi ya Europa. Akiwa ndio kwanza ana umri wa miaka 33 wakati akichukua ajira hiyo, aliahidi kuibadili Chelsea kwa kuleta vijana lakini alionyeshwa mlango wa kutokea baada ya Chelsea kulala 3-1 ugenini dhidi ya Napoli katika Ligi ya Klabu Bingwa na huku akiachwa kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.
ROBERTO DI MATTEO (Machi 2012-Novemba 2012)
Di Matteo alichukua timu kama kocha wa muda lakini aliiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa KombFA kabla ya kushinda kwa matuta fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich na kuipa timu hiyo ubingwa wa kwanza Ulaya katika historia yao. Akapewa ajira ya kudumu Juni. Msimu wake wa kwanza kamili ukaanza kwa kishindo lakini Muitalia huyo maarufu alitimuliwa baada ya mwendo mbovu wa kiwango uliowaacha wakiwa hatarini kuaga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa huku wakiwa wameshuka kutoka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.hadi nafasi ya tatu.
NB: Ray Wilkins alifanya kama kocha wa muda kwa mechi moja katika msimu wa 2008-09.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment