Sofia Simba akishangilia baada ya kujua kuwa 'amemgaragaza' vibaya mpinzani wake Anne Kilango Malecela katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa UWT mjini Dodoma. |
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi
(UWT), Sophia Simba, ameibuka kidedea ambapo ametetea kiti chake kwa kumbwaga
mpinzani wake mkubwa Anna Kilango Malecela kwa zaidi ya nusu ya kura
zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu wa jumuiya hiyo uliofanyika jana mjini hapa.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi huo,
Abdulhamani Kinana, alimtangaza Simba, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto kuwa mshindi wa kiti hicho.
Jumla ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo zilikuwa 1,038
na mbili kati ya hizo ziliharibika ambapo Simba alizoa kura zaidi ya 700 huku
mpinzani wake akipata kura zaidi ya 300 na nafasi ya mwisho ikishikiliwa
na MayRose Majinge, aliyeambulia kura
saba.
Awali uchaguzi huo ulitawaliwa na mizengwe baada ya Simba na
Mbunge wa Afrika Mashariki, Shyrose
Banji, kutaka kuchapana makonde.
Aidha, posho za wajumbe kutoka mkoa wa Pwani zilitangazwa
kuibiwa katika mkutano huo.
Hali hiyo ilitokea muda mfupi jana baada ya Simba kujibu
swali lililoulizwa na Bhanji, akimtaka aeleze wapiga kura atawezaje kukivusha
chama katika uchaguzi mkuu ujao ikiwa haonekani katika majukwaa ya siasa
kuhamasisha wanawake kujiunga na umoja huo.
Hata hivyo, Bhanji alipata wakati mgumu baada ya kukatishwa
mara kwa mara na kelele za wajumbe walionekana kukerwa na swali lake.
Akijibu swali hilo Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, alisema Bhanji hajui siasa za chini kwa chini.
Alisema yeye ni serikali kwa hiyo hawezi kuikosoa serikali
bungeni,” Siwezi kukikosoa chama changu bungeni. Wabunge wa CCM hawatakiwi
kukikosoa chama chako kwa mithili ya kukiangusha.”
Alisema mwaka 2010 walihangaika yeye na Baraza lake kupita
nchi nzima kuomba kura kwa wananchi na kwamba Rais Jakaya Kikwete alikiri kuwa
ushindi huo umeletwa na wanawake.
“Mimi ndio kamanda wenu nichagueni mimi…. Huyu amepata
ubunge wa Afrika Mashariki hivi karibuni hajui huko chini mmefanya nini CCM,”
alisema na kushangiliwa na wajumbe.
Baada ya kumalizika kwa Swali hilo, Mwenyekiti wa mkutano
huo ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka, alimtaka kwenda kuchukua nafasi yake na hapo
ndipo wapambe wa Simba kutoka Mkoa wa
Dar es Salaam walipomtaka Bhanji aliyekaa katika kiti cha mgombea huyo
kuondoka.
Hata hivyo, alipofika katika eneo hilo, Simba alimtupia
kijembe Bhanji, “ huniwezi wewe’ hali iliyomfanya Bhanji kuhamaki na kutaka
kusikia tena “what” ( nini).
Kutokana na kuhamaki huko,
baadhi ya wajumbe waliinuka na kwenda kuamulia kwa kumshawishi Bhanji
kutoka katika eneo hilo kwa ajili ya usalama.
Aidha, katika mkutano huo, Mshereheshaji ambaye ni
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu, alitangaza kuibiwa kwa posho za
wajumbe wa mkutano wa mkoa wa Pwani zaidi ya 40.
“Waheshimiwa wajumbe kuna mtu amechukua mkoba ambao si wake,
ulikuwa na posho za wajumbe naomba jamani aliyechukua arudishe ili wenzenu
waweze kupata posho,”alisema.
Awali kabla ya kuanza kujieleza kwa wagombea wa nafasi hiyo, Profesa Tibaijuka, alitaka kuanza kujieleza kwa wagombea hao, ambapo alianza kuja majina ya wagombea
watatu.
“Ataanza MayRose Majinge, Anne Malecela Kilango na kufuatiwa
na Sophia Simba ambaye mambo yake tumeshayaona hapa,”alisema.
MAJINGE
Alisema kuvaa khanga na kuimba nyimbo sio kigezo cha
kumchagua mgombea bali wanatakiwa waangalie maendeleo.
“Mimi ninatosha katika maarifa, taaluma na kimaadili,
nitumeni mimi nikawatumikie,” alisema.
MALECELA
Malecela ambaye awali alisindikizwa na mumewe, Mzee John
Malecela hadi mlangoni ambapo alimbusu kama ishara ya kumtakia uchaguzi mwema,
aliingia katika eneo la kipaza sauti akiwa ameshikilia biblia yake mkononi.
Alisema uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa mgumu hivyo
kunahitajika kiongozi madhubuti
atakayeweza kuivusha CCM katika uchaguzi huo.
Alisema uwezo wa kukijenga chama anao na uwezo wa kukivusha
chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Pia alisema anaumia sana na suala la watendaji wa chama
hicho kutenganishwa kikazi na wenza wao, jambo ambalo linawafanya ndoa zao kuwa
mashakani.
Alisema kuwa kwa
kusaidiana na wenzake, atatafuta njia ya kuwawezesha watendaji hao kuishi
katika eneo moja.
SOPHIA SIMBA
Alisema ukomo ulioamuliwa ulikuwa ni kwa upande wa ubunge wa
viti maalum tu na wala si kwa madiwani.
Alisema suala hilo litaamuliwa na wanawake wa CCM na wale walio nje ya chama
hicho katika utungaji wa katiba mpya.
Pia alisema umoja huo uko mbioni kujenga jengo la ghorofa 16
ambalo litajulikana kama Mama Nyerere Tower.
Dk. GHALIB MOHAMMED BILAL
Awali akifungua mkutano, Makamu wa Rais, Dk Gharib Mohammed
Bilal, aliwataka wajumbe hao kutochagua viongozi waliojaa rushwa na wale
wanaonunua uongozi.
“Uongozi ni utumishi sasa wale wanaonunua maana hawataki
kuja kututumikia. Ni marufuku kabisa kwenu na chama kwa ujumla kuwa nyinyi ni
madalali wa rushwa,” alisema na kuongeza:
“Hao wanaowanunua muwaulize wamegundua mtaji gani huko? Kwa
hiyo yeyote mnaedhania tu kuwa katumia rushwa msimpe uongozi.”
HALI KABLA YA MKUTANO
Katika nje ya ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini hapa,
kulikuwa na makundi mawili yaliyokuwa yakirushiana tambo na vijembe vya kila
aina kwa wapambe wa wagombea wawili (Simba na Malecela).
Wapambe wa Malecela walisikika wakiimba kuwa wanataka
mabadiliko huku wale wa Simba wakisema hawataki mabadiliko.
Mgombea wa kwanza kuwasili katika viyunga vya ukumbi huo,
alikuwa Simba ambaye alisimama getini akiomba kura kutoka kwa wajumbe wa
mkutano huo, huku Majinge akionekana akifuata mjumbe mmoja mmoja mahali
alipoketi.
Hali ilikuwa sawa kwa Malecela aliyekuwa pia akiwafuata
wajumbe walipokaa na kuowaomba kura.
RUSHWA
Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takukuru), walipiga kambi katika
vyoo vya ukumbi huo wa mkutano ili kudhibiti rushwa.
“Kila saa mnaingia chooni na kurudi, tupo hapa
tunawaangalia,”alisikika mmoja wa watu
wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Takukuru.
Chanzo: Nipashe Jumapili
No comments:
Post a Comment