![]() |
Marehemu Liberatus Barlow enzi za uhai wake. |
![]() |
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela. |
![]() |
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani
|
![]() |
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe |
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Stephen Zelothe
|
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo |
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, aliwaambia
waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa Barlow, aliuawa maeneo ya Kitangiri katika barabara
inayoelekea Bwiru, jirani na hoteli ya Tai Five jijini hapa.
Alisema mauaji hayo yalifanyika kati ya saa 7 na saa 8
usiku, wakati Barlow akimsindikiza mwanamke aliyejulikana kama
Doroth Moses.
Inasemekana kuwa wote wawili, walikuwa wametoka kuhudhuria
kikao cha maandalizi ya harusi ya mtoto wa dada wa Barlow, kilichofanyika
hoteli ya Florida.
Hata hivyo, taarifa zisizo rasmi kutoka mitandao ya kijamii
kuhusu utata wa mauaji hayo, zinaeleza kuwa Barlow na mwanamke huyo walikuwa
wanatoka katika hoteli inayotajwa kwa jina la La-Kairo.
Akifafanua, Ndikilo alisema Barlow alikuwa akiendesha gari
yake binafsi aina ya Toyota Hilux- double cabin na kwamba alikuwa akimsindikiza
mwanamke huyo kwenda nyumbani kwake.
Mwanamke huyo ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano
zaidi, ni mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana.
Alisema wakati wakikaribia eneo la Kitangiri anakoishi
mwanamke huyo, waliwaona watu wawili wakiwa wamevaa mavazi maalum (jackets)
yanayovaliwa na wananchi wanaoshiriki ulinzi shirikishi unaofahamika pia kama polisi jamii.
Kwa mujibu wa Ndikilo, baada ya kuwaona watu hao ambao
waliwamulika kwa tochi, Doroth alimuuliza Barlow iwapo anawafahamu, naye
alimjibu kuwa watakuwa ni polisi jamii.
Hata hivyo, Ndikilo alisema baada ya Barlow kusimamisha gari
pembeni, mkabala na nyumba anayoishi mwanamke huyo, watu hao wawili
waliwasogelea huku wakionyesha kukerwa na mwanga wa taa za gari.
Alisema watu hao walimhoji Barlow kwa nini anawamulika kwa
taa za gari, lakini wakati akijaribu kutoa ufafanuzi kwamba yeye ni RPC, ghafla
walitokea watu wengine wapatao watatu, walisimama kuzunguka gari la Kamanda
huyo.
Baada ya kuona hali hiyo, huku akijaribu kuwauliza iwapo
hawamfahamu kuwa yeye ndiye RPC na kutoa radio call (simu ya upepo) ili kufanya
mawasiliano na polisi wa doria.
“Ghafla mmoja wa watu hao alitoa bastola na kumfyatulia
risasi ambayo iliingilia shingoni na kutokea upande wa pili wa bega,” alisema
Ndikilo.
Alisema baada ya tukio hilo,
watu hao walichukua vitu kadhaa ikiwemo bastola, simu na radio call alivyokuwa
navyo Barlow na kutoweka kusikojulikana.
“Kimsingi mazingira ya mauaji yenyewe bado yana utata,
lakini Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
tunafanya kazi ya kuchunguza ili kuujua ukweli,”alisema.
Kwa mujibu wa Ndikilo, baada ya kufyatuliwa risasi
inaaminika Barlow alikufa papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi na mwili
wake umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando ukisubiri taratibu za
mazishi.
Alisema kutokana na mazingira hayo ya utata ya mauaji, Jeshi
la Polisi linamshikilia mwanamke aliyekuwa naye kwa mahoajiano zaidi.
Taarifa za awali zilidai kwamba mwanamke huyo anayesadikiwa
kuwa ni mjane, ni dada yake Barlow.
Lakini baadaye jana, Mkuu wa mkoa wa Mwanza alikanusha
taarifa hizo na kusisitiza kuwa ni mtu ambaye alikuwa amempa lifti wakati
wakitoka katika kikao cha harusi.
Kufuatia mauaji hayo Ndikilo alisema kuwa Polisi Makao
Makuu, limemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert
Manumba kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Nyumbani kwa Doroth, kijana Kenrogers Edwin
aliyejitambulisha kama mtoto wa kaka yake wa mwanamke huyo, alisema kabla ya
tukio hilo,
shangazi yake (Doroth) alipiga simu ili wamfungulie geti.
Alisema kwamba wakati akifungua geti, aliona gari likiwa
limeegesha huku watu wawili wakiwa upande wa abiria na wengine watatu wakiwa
upande wa dereva na kisha alisikia mlio wa risasi na baadaye watu hao walitimua
mbio baada ya kuona pikipiki inakuja
nyuma yao.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia mauaji hayo walielezea
kushangazwa kwao na hatua ya Barlow kutembea usiku bila mlinzi wake (bodyguard)
ambaye kwa kiwango kikubwa angeweza kusaidia kumuepusha na kifo.
IGP MWEMA AMTUMA DCI KWA UPEPELEZI
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, katika taarifa
aliyoitoa jana jijini Dar es Salaam, alisema
ameshamtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba,
mkoani humo kuimarisha ulinzi na upepelezi wa tukio hilo.
Aidha, Mwema amewaomba wananchi kuwa watulivu na kutoa
ushirikiano kwa jeshi hilo,
utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao.
Akielezea kuhusu mauaji hayo, Mwema alisema, wakati huo
Barlow alikuwa akitokea kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la Florida hoteli Mwanza
mjini.
Alisema alikuwa ameongozana na ndugu yake wakitoka kwenye
kikao hicho.
Alisema tukio hilo
limewashtua na kuwahuzunisha na kwamba wakati uchunguzi ukiendelea, wataendelea
kutoa taarifa kadri wanakavyozipata.
….MAKAMANDA WA MIKOA WATOA KILIO
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya makamanda wa
polisi wa mikoa mbalimbali nchini, wamesema kuwa wamempoteza kiongozi mwenye
uzoefu wa muda mrefu kazini na aliyekuwa mchapakazi katika jeshi hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela,
alisema ukomavu wa kazi ndio uliosababisha kamanda huyo kupelekwa katika mkoa
ambao ni miongoni mwa mikoa migumu nchini.
Alisema enzi za uhai wake, alikuwa akiwaelimisha wenzake ili
waweze kufanya kazi kwa ufanisi na
kwamba alikuwa mwepesi kuwarekebisha wale wanaoenda kinyume na kazi.
Kenyela alisema kwa upande wake atamkumbuka kwa sababu ndiye
aliyempokea wakati akianza kazi hiyo na alikuwa akiishi naye kwenye kambi za
maofisa huko Tabata.
“Wito wangu kwa wananchi walaani vitendo vya mauaji ya
viongozi kwa sababu kumpoteza kiongozi ni gharama kubwa katika nchi hasa
ukiangalia muda uliotumika kumuandaa hadi amefikia hatua hii,” alisema.
MOROGORO
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema kuwa, ameguswa na msiba
huo wa ghafla na kueleza kuwa, atamkumbuka daima kwa kuwa alikuwa akifanya kazi
yake kwa kujiamini.
“Tumempoteza jembe kwa sababu alikuwa mzoefu kwenye kazi na
asiye mchoyo pindi umwombapo ushauri, kwa wale wachanga kwenye kazi walikuwa
wakimtumia sana ili waweze kuifanya kazi yao kwa ufanisi,”
alisema.
MTWARA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki amewataka
wenzake, kuyaenzi na kuyaendeleza yale mazuri aliyokuwa akiyafanya Barlow enzi
za uhai wake.
TANGA
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe,
ameeleza kusitikitishwa na mauaji ya Barlow na kuwataka watumishi wa jeshi hilo
kuwa wavumilivu wakati wakisubiri uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ili hatua
madhubuti ziweze kuchukuliwa.
“Kwa sababu kuna kikosi maalum ambacho kimeenda kufanya
uchunguzi wa mauaji hayo basi nawasihi wenzangu tuendelee kuwa wavumilivu mpaka
hapo upelelezi utakapokamilika na kujua hatma yake au hatua gani za kuchukua,
“alisema.
Alimwelezea marehemu alikuwa mtu mchapa kazi, mvumilivu na
aliyeipenda kazi yake na kwamba ameacha pengo kubwa katika nafasi hiyo.
KILIMANJARO
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Robert Boaz, amesema kifo cha Barlow ni cha kawaida ambacho kinaweza kumkuta mtu yeyote na haipaswi kujiuliza maswali
mengi.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Boaz alisema
kifo
hicho kinaweza kikamkuta hata rais wa nchi yoyote ambaye
analindwa na walinzi chungu nzima.
“Kifo chake kinatupa majonzi sisi makamanda wenzake,lakini
kikubwa kilichobaki ni kumuombea kwa Mungu na kuacha uchunguzi kufanyika,” alisema.
Aliongeza, “kwa sasa ni mapema mno kuzungumza
chochote,lakini
ninachoweza kusema ni kuwa kifo chake kimenistua na ni kifo
ambacho kinaweza kikamtokea mtu yeyote.”
Aidha kwa upande wao baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro
wameeleza kushangazwa na kiongozi mkubwa wa Polisi kuuawa na
majambazi.
Bariki Sanga mkazi wa Kilimanjaro aliliambia NIPASHE
Jumapili kuwa,ni jambo la kujifunza kwa kila kiongozi na kila raia kuwa mlinzi
wa mali
zake mwenyewe
MBEYA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, amesema
amepokea kwa mshtuko na masikitiko kifo hicho.
Alisema ingawa hapaswi kulitolea tamko kwa kuwa
linashugulikiwa na Polisi Makao Makuu, kifo hicho ni changamoto kubwa kwa jeshi
hilo ambalo
sasa linatakiwa kujipanga na kufanya kazi kwa bidii.
Alisema kuwa yeye binafsi anamfahamu vizuri Barlow kwa kuwa
alimpokea vizuri wakati yeye (Diwani) alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa
Kamanda wa Polisi wa mkoani Shinyanga.
Alisema Barlow pia alikuwa ni mwenyekiti wa Makamanda wa
Polisi wa Kanda ya Ziwa ambaye alikuwa akiwaunganisha vizuri na kupunguza
kabisa matukio ya uhalifu kwenye kanda hiyo.
Aliongeza kuwa kwa vyovyote ambavyo uchunguzi utakavyobaini,
kifo cha Barlow ni pigo kwa Polisi, kwa kuwa mchano wake ulikuwa bado
unahitajika sana ndani ya jeshi hilo.
DODOMA
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Stephen Zelothe, ambaye
Barlow alikuwa mwanafunzi wake kikazi,
alisema ni masikitiko makubwa kutokea kwa tukio hilo.
“Ni masikitiko makubwa kutokea kwa jambo hili…siwezi kusema
lolote tuache kwanza mambo ya kidunia (mazishi) yapite,”alisema Zelothe kwa
masikitiko makubwa alipoulizwa nini kifanyike
(Chanzo: NIPASHE JUMAPILI)
No comments:
Post a Comment