Marcelo anavyoonekana na 'hogo' lake leo (Oktoba 16, 2012) baada ya kuvunjika mfupa wa mguu akiwa mazoezini na timu ya taifa lake la Brazil. |
MADRID, Hispania
FIFA italipa mshahara wa Marcelo
katika kipindi chote atakachokuwa nje kutokana na majeraha kupitia sheria mpya
inayozilinda klabu, ambayo imeanza kutumika rasmi Mei mwaka huu.
Katika mpango huo wa bima, FIFA
itakuwa ikizilipa fidia klabu ambazo wachezaji wake wataumia wakati
wakizitumikia timu za mataifa yao wakati wa michuano ya kimataifa.
Klabu ambazo zitashindwa kuwatumia
wachezaji wake kwa siku 28 mfululizo au zaidi kutokana na majeraha, kama ilivyo
kwa Marcelo atakayekosekana Real Madrid kwa miezi mitatu, zitakuwa na haki ya
kudai fidia kupitia mpango huo, ambao unatoa fidia ya juu kwa siku kuwa ni euro
20,548 (Sh. milioni 40). Kiwango hiki cha ukomo kimewekwa kwa kuzingatia bajeti
yote ya jumla ya mpangp huo ambayo ni euro milioni 60 (Sh. bilioni 120).
Kiwango cha fidia huzingatia mshahara
wa mchezaji katika klabu yake kama mfanyakazi, hii ikimaanisha kuwa ni pamoja
na kiwango anacholipwa kwa wiki au kwa mwezi, pamoja na malipo yote ya huduma
za kijamii.
Kwa kuzingatia kwamba Marcelo hulipwa
euro milioni 2.3 (Sh. bilioni 4.6) kwa mwaka baada ya kukatwa kodi, FIFA
italazimika kuilipa Real Madrid euro 6,300 kwa siku (Sh. milioni 12.7) hadi
beki huyo wa kushoto atakapopona na kurejea uwanjani kwa ruhusa ya madaktari.
Hivi sasa Real Madrid bado wanasubiri
kujua ni kwa muda gani beki huyo wa kimataifa wa Brazil atakuwa nje baada ya kuumia wakati akiwa mazoezini.
Wakilipwa na FIFA kwa miezi mitatu ya
kuwa nje kwa Marcelo kama inavyotazamiwa,
Real Madrid wataingiza fedha za ziada kupitia mpango huo kiasi cha euro
574,000 (Sh. bilioni 1.2).
No comments:
Post a Comment