TIMU ya Yanga yenye maskani yake katika Mtaa wa Jangwani Jijini Dar es Salaam imefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kampuni ya bia, Tanzania Breweries Limited (TBL), kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Akiongea katika ziara hiyo afisa habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema timu yake imeamua kufanya ziara yao katika kiwanda hicho ili kujionea mambo mbalimbali yanayofanywa na kampuni hiyo inayozalisha vinywaji mbali mbali pamoja na bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo ndio wadhamini wakuu wa timu hiyo.
Alisema kuwa Kilimanjaro Premium Lager imekuwa ikiwapa ushirikiano mkubwa katika mambo mbalimbali ya kimichezo ikiwa ni pamoja na kuwapatia magari ya usafiri jezi pamoja na vifaa mbalimbali vya michezo, na wamefurahishwa sana na jinsi walivyopokewa vizuri kiwandani hapo na aliwaomba waendelee na moyo huo wa kuthamini timu yao.
“Tunawaomba muendele na moyo huo huo kwani sisi kama Yanga, tunaamini kuwa huwezi kutenganisha mafanyikio ya Yanga na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager na kwamba kwa pamoja, tutaweza kulifikisha soka la Tanzania katika kilele cha ubora,” alisema Sendeu.
Awali, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kuwa wamefurahishwa sana na kitendo cha timu hii ya Yanga kuamua kuacha shughuli zao na kutembelea kiwanda chao na kujionea kazi za uzalishaji zinavyofanywa kiwandani hapo.
Alisema kuwa Kilimanjaro Premium Lager inathamini mchango wa timu za Yanga kwa soka la Tanzania na ndio maana imekuwa ikiidhamini timu hio huku akibainisha kuwa wataendela kudhamini timu ya Yanga kwa muda mrefu.
Hivi sasa, thamani ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa timu za Yanga unafikia jumla ya dola za Kimarekani milioni 1.5 (Sh. bilioni 2) kwa mwaka kwa kila timu. Pesa hizi hutolewa kwa ajili ya shughuli mbali mbali kama kusajili wachezaji wapya wenye viwango vya kimataifa, mabasi , vifaa vya michezo na kukiwezesha Mkutano Mkuu wa Mwaka na kuijengea uwezo timu ya Yanga.
“Tunafanya hivi tukiwa na nia ya kupeleka soka la Tanzania kwenye kilele cha mafanikio… Ni dhahiri kuwa timu ya Yanga imekuwa ikifanyia mambo makubwa kwani imekuwa ikiwapatia vijana mbalimbali ajira kupitia timu yao. Ushirikiano wetu na timu ya Yanga inatokana na ukweli kwamba Yanga ndio kati ya timu zenye wapenzi wengi zaidi hapa nchini… timu ya Yanga pia ndio kati ya timu yenye historia yakipekee hapa nchini na inachangia wachezaji wengi kwenye timu ya Taifa Taifa Stars,” alisema.
Aliwasihi wananchi kwa ujumla na haswa washabiki wa Yanga kuendelea kuisapoti timu kufuatana na mafanikio yake kwenye ligi na mchango wake kwenye timu ya Taifa na aliitakia timu ya Yanga kila la heri kwenye msimu wa 2012/2013.
Kavishe alisema ndoa kati ya Kilimanjaro Premium Lager ni yenye mafanikio kwani ndani ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager, timu hiyo imejipatia ubingwa katika mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mwaliko kutoka Ikulu ya Tanzania na ile ya Rwanda baada ya kushinda ubingwa wa michuano ya Kagame kwa misimu miwili mfululizo.
No comments:
Post a Comment