Gonzalo Higuain (kushoto) akishangilia goli la kusawazisha alilofunga dhidi ya Peru |
Gonzalo Higuain (kulia) akishangilia goli la kusawazisha alilofunga dhidi ya Peru pamoja na Messi (kulia) na Angel di Maria. |
Fernando Gago wa Argentina akitolewa kwa machela baada ya kuumia wakati wa mechi yao dhidi ya Peru. |
BUENOS AIRES, Argentina
MFULULIZO wa magoli mengi kutoka kwa Lionel Messi ulisimamishwa alfajiri ya leo katika sare isiyovutia ya Argentina ya 1-1 dhidi ya Peru huku Colombia wakizidi kung'aa katika Kundi la Amerika Kusini la kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Argentina inaongoza kundi hilo lenye mataifa tisa juu ya Colombia na Ecuador lakini ni pointi tatu tu zinazozitofautisha timu sita za juu huku mfululizo wa mechi za kukamilisha nusu ya kwanza na mzunguko ikitarajiwa kuwa mwezi ujao.
Peru walianika udhaifu wa safu ya ulinzi ya Argentina kwamba safu yao kali ya ushambuliaji huwa inayumba pia katika mazingira magumu ya uwanja Estadio Nacional mjini Lima.
Goli tamu la kusawazisha la Gonzalo Higuain lilikuwa ni moja ya mambo machache ya kuvutia yaliyoanywa na Argentina katika mechi ambayo ilishuhudia kipa wao Sergio Romero akidaka penalti ya mapema kutoka kwa Claudio Pizarro.
Ilikuwa ni ngumu kuamini kama Messi alikuwa ni mchezaji bora wa dunia, akitulizwa na rafu za mapema lakini hakuchezewa kibabe sana katika ulinzi wa "mtu kwa mtu" kama aliokumbana nao Diego Maradona wakati walipolala 1-0 katika mji mkuu wa Peru miaka 27.
Alidhibitiwa "msitu" wa viungo wa Peru, ambao bado waliweza kuleta madhara langoni mwa Argentina huku beki Carlos Zambrano akifunga katika dakika ya 22 na Luis Ramirez akigongesha nguzo katika kipindi cha pili.
"Dimba la kuchezea lilikuwa ovyo na halisapoti mchezo, huwezi kuumiliki mpira hadi kwanza uuguse mara moja au mbili zaidi. Tulikerwa na uwanja kwa sababu hatukuweza kucheza kwa staili yetu lakini hata hivyo sare ni nzuri," Messi, ambaye alifunga magoli 10 katika mechi zake sita zilizopita za kimataifa, aliwaambia waandishi wa habari.
"Tuna hasira kwamba tuna pointi saba tu wakati tulistahili zaidi," alisema kocha wa Peru raia wa Uruguay, Sergio Markarian, ambaye anajaribu kuisaidia timu hiyo kufuzu kucheza fainali za dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1982.
"Peru hawakunishangaza. Siku hizi, kila mechi ni ngumu, daima ngumu sana," kocha wa Argentina, Alejandro Sabella alisema kuhusu matokeo hayo na msimamo wa kundi kuwa mgumu.
Argentina wana pointi 14, Colombia na Ecuador 13, Uruguay na Chile 12 naVenezuela, wanaojaribu kufuzu kwa mara ya kwanza wana pointi 11.
Mwisho wa kampeni hizo ndefu, timu nne za juu zitafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 na mshindi wa tano ataingia katika "kapu" dhidi ya taifa la bara la Asia kuwania kwenda Brazil.
FALCAO ATUPIA TATU
Colombia, yenye nyota kama Radamel Falcao na Teo Gutierrez ambao kila mmoja amefunga magoli matatu katika mechi mbili, ikiwamo waliyoshinda 4-0 dhidi ya Uruguay Ijumaa, jana walishinda 3-1 ugenini dhidi ya timu iliyocharuka ya Chile mjini Santiago.
"Timu ilikuwa ikijiamini licha ya kutanguliwa katika kipindi cha kwanza," kocha wa Colombia, Jose Pekerman alisema.
"Kujiamini huku kumekuwa ni muhimu sana kwetu na kumethibitisha kwamba timu hii inakuja vizuri. Hii ilikuwa moja ya mechi ngumu zaidi unazokumbana nazo katika kuwania kufuzu."
Akisifiwa kwa kuifufua Colombia baada ya mwanzo mbaya wa kocha aliyefukuzwa Leonel Alvarez, Muargentina huyo alisema siri ya mafanikio yao ni kutumia kipindi cha wikiendi ya mechi za kimataifa za FIFA mwezi Agosti kujifua badala ya kucheza mechi ya kirafiki.
"Ratiba hii imetubeba sana na nadhani sasa tunakula matunda ya kazi yetu lakini ilikuwa ikiuma sana wakati (shutuma) zilipokuwa zikikiminika kuonyesha kutoeleweka kwa kazi yetu," alisema.
Katika mechi
nyingine mbalimbali za hatua za awali za Kombe la Dunia, Hispania walishinda
1-0 dhidi ya Georgia, Austria 1 Ujerumani 2, Italia 2 Malta 0, England 1
Ukraine 1, Ufaransa 3 Belarus 1, Israel 0 Urusi 4, Hungary 1 Uholanzi 4, Serbia
6 Wales 1, Bosnia 4 Latvia 1, Ugiriki 2 Lithuania 1, Bulgaria 1 Armenia 0, Ureno 3 Azerbaijan 0, Uswisi 2 Albania 0 na Ubelgiji 1 Croatia 1.
------
No comments:
Post a Comment