Nahodha wa Simba akinyanyua juu Ngao ya Jamii waliyotwaa baada ya kuifunga Azam 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi |
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo ni mdhamini wa klabu za Simba na Yanga, imeipongeza Simba kwa kutwaa Ngao ya Hisani mara mbili mfululizo na kusema ni ishara nzuri ya matokeo mengine mazuri katika ligi kuu inayotarajiwa kuanza Jumamosi hii.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alisema, “Tumefurahishwa sana kwa ushindi huu wa Simba kwani ni ishara kuwa wamepania kutetea ubingwa wao vilivyo msimu huu.”
Alisema mchezo wa Simba dhidi ya Azam ulikuwa mkali na wenye ushindani mkubwa lakini Simba ilionyesha uwezo mkubwa na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
“Siku zote sisi Kilimanjaro Premium Lager tunajihusisha na ushindi na ndio maana tumepania kuifikisha soka ya Tanzania katika kilele cha mafanikio,” alisema Kavishe na kuongeza kuwa nia yao kama wadhamini ni kuendelea kuona timu hizi zinafanya vizuri katika ligi kuu na mashindano mengine yakiwamo ya kimataifa.
Katika taarifa yake meneja huyo alitoa rai kwa timu ya Yanga pia kuhakikisha inaanza mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Prisons vizuri huko Mbeya wakati Simba itamenyana na African Lyon Jijini Dar es Salaam.
“Tunatumai kuwa timu hizi, zinazodhaminiwa na bia yetu ya Kilimanjaro Premium Lager, zitaonyesha nidhamu ya hali ya juu wakati wa ligi hii na kuleta ushindani mkubwa kama ilivyo miaka yote,” alisema Kavishe.
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kukabidhi mabasi ya kisasa kwa timu hizo mbili hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment