Tuesday, August 7, 2012

ZAKIA MRISHO NAYE AFUNGASHWA VIRAGO OLIMPIKI, NI BAADA YA KUSHIKA NAFASI YA 31 LEO KATI YA WAKIMBIAJI 36 MITA 5,000

Usijali mama, kutolewa mapema kimataifa nd'o zetu... ! Zakia Mrisho akibeba bendera ya taifa  kuongoza wanamichezo wenzake wa timu ya Tanzania katika siku ya ufunguzi wa michezo ya  Olimpiki jijini London, Julai 27, 2012.
LONDON, England
AMA kweli aliyeturoga Watanzania katika sekta ya michezo kafa. Kwa mara nyingine tena, mwanamichezo Zakia Mrisho aliyekuwa akipeperusha bendera ya Tanzania katika michezo ya Olimpiki jijini London amefungashwa virago mapema baada ya kushika nafasi ya 31 kati ya wanariadha wa kike 36 waliokuwa wakichuana leo katika hatua ya mchujo wa mbio za mita 5,000.

Katika kuonyesha kwamba safari yetu bado ndefu sana kukaribia waliko jirani zetu kama Kenya, Zakia alishika nafasi ya 16 kati ya wakimbiaji 18 wa kundi lake, akitumia muda wa 15:39:58 na hivyo kuwazidi wanariadha wawili tu walioshika mkia!

Zakia ni mwanamichezo wa nne wa Tanzania kuaga mapema katika michezo hiyo baada ya kudundwa vibaya kwa bondia Selemani Kidunda na kuchemsha kuliko kawaida kwa waogeleaji Magdalena Moshi na Ammar Ghadiyal.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, mkuu wa msafara wa timu ya wanamichezo wa Tanzania inayoshiriki Olimpiki jijini London 2012,  Hassan Jarufu, alisema kuwa sasa matumaini yao yamebaki kwa Samson Ramadhan, Faustine Mussa na Mohamed Msenduki ambao watashuka dimbani Agosti 12 katika mbio ndefu za Marathon.

Katika michezo hiyo, Tanzania ilipeleka washiriki 7.

No comments:

Post a Comment