Serge Ombomo (kulia) ni mmoja wa mabondia waliozamia |
WANAMICHEZO saba wa Cameroon wametoweka wakati wakiwa katika Michezo ya Olimpiki nchini Uingereza, maafisa wamesema.
David Ojong, mkuu wa msafara wa Cameroon, amesema mabondia watano, muogeleaji mmoja na mcheza soka mwanamke mmoja wametoweka tangu wikiendi.
Sababu ya kutoweka kwao haijajulikana, lakini inahisiwa kwamba wanataka kubaki Uingereza kwa sababu za kiuchumi.
Ojong alisema wanamichezo hao wana viza za kukaa nchini humo hadi Novemba.
"Kilichoanza kama uvumi hatimaye kimekuwa kweli," Ojong alisema, katika barua aliyoiandika kwa wizara ya michezo ya Cameroon.
"Wanamichezo saba wa Cameroon walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya London 2012 wametoweka kutoka katika Kijiji cha Olimpiki."
Kipa wa akiba wa timu ya soka ya wanawake, Drusille Ngako, alikuwa wa kwanza kutoweka, kwa mujibu wa Ojong.
Alitoweka wakati wachezaji wenzake walipoondoka kwenda Coventry kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya mwisho dhidi ya New Zealand, alisema.
Kutoweka kwake kulifuatiwa na kutoweka kwa muogeleaji Paul Ekane Edingue, akiripotiwa kubeba kila kilicho chake.
Mabondia watano ambao walitolewa katika mapambano yao walitoweka kutoa katika Kijiji cha Olimpiki cha London Jumapili, Ojong alisema.
Aliwataja kuwa ni Thomas Essomba, Christian Donfack Adjoufack, Abdon Mewoli, Blaise Yepmou Mendouo na Serge Ambomo.
Wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza ilisema haiwezi kuzungumzia kama yupo kati ya saba hao aliyeomba kuishi nchini humo, shirika la habari la Associated Press liliripoti.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habarri, tukio hilo si la kwanza la aina hiyo, kwani ubalozi wa Sudan ulithibitisha mwezi uliopita kwamba wanariadha watatu walitoweka.
Mmoja ameomba kuishi nchini humo na wengine wawili wanatarajiwa kufanya hivyo pia, iliripoti AP.
No comments:
Post a Comment