Klabu ya Azam FC
inapenda kutoa taarifa ya ufafanuzi juu ya sakata la mchezaji Mrisho Ngassa
ambalo linaonekana kupotoshwa
Azam FC ilitangaza
kuwa biashara ya mchezaji Mrisho Ngassa ingefungwa siku ya Jumatano 1/08/2012
saa saba mchana na ilizitaka klabu zenye 'interest' na mchezaji huyo kufika
makao makuu ya Azam FC, ofisi ndogo zilizopo kwenye kiwanda cha unga cha
Azam-Mzizima zikiwa na pesa taslimu. Bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni dola
za Marekani 50,000. Lakini katika mawasiliano ya 'email' kwa makatibu wakuu wa
Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei ya
mauzo na ingemuuza Ngassa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya
mwenzake.
Kwa maana hiyo
biashara ya mchezaji Mrisho Ngassa ilifanyika kwa uwazi. Lengo la Azam FC
lilikuwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata
huduma ya Ngassa.
Pia tunaomba
ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngassa alipewa taarifa kuwa anauzwa na
aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake. Ngassa
alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona
imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na
Azam FC yazingatiwe.
Hadi kufikia siku ya
Jumatano 01/08/2012 saa saba mchana, ni klabu ya Simba pekee iliyojibu kwa
maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngassa. Yanga wao hawakuwahi kujibu
'email', ingawa kwa majibu ya simu mjumbe wao wa kamati ya usajili, Seif
'Magari' alitangaza kuwa Ngassa hana thamani ya zaidi ya Sh. milioni 20. Na Yanga
haikuwa tayari kuboresha ofa yake.
Muda wa kufungwa kwa
biashara ya kumuuza Ngassa ulipofika, ni Simba pekee kupitia kwa makamu
mwenyekiti wake Geofrey Nyange 'Kaburu' na mhasibu wake ndio waliofika wakiwa
na pesa taslimu Sh. milioni 25. Yanga hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata
simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana 'interest'.
Kikao cha dharura cha
Azam FC kilikaa na kuamua kuwa biashara ya kumuuza Ngassa ilishindikana
kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000. Kwa maana hiyo Azam
FC iliamua kumpeleka Ngassa kwa mkopo kwenye klabu iliyofika na kuonesha nia ya
kumhitaji (Simba).
Simba walipewa sharti
la kuhakikisha wanamlipa Ngassa mshahara wake kamili (Sh.milioni 2) pamoja na
stahiki zake nyingine zote za kimkataba.
Sababu za kumpeleka
Ngassa kwa mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam ingetoa kwa
Ngassa kama angebaki.
Azam FC inapenda
kuweka wazi kuwa haijamlazimisha Ngassa kwenda Simba kama inavyopotoshwa. Kama
Ngassa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na
dola 50,000 na Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo
Simba lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC.
Tunaomba kuweka
msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngassa na kuvunja mkataba wake na
hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngassa hataki kwenda tunakompeleka Azam FC
inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu.
Lakini Ngasa na
washauri wake waelewe kuwa akiamua kubaki Azam FC atakaa nje ya uwanja kwa muda
wote uliosalia kwenye mkataba wake, kwani Azam FC haipo tayari kumvisha jezi
mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
Kwa kuwa sakata hili
limeanza kuhusishwa na sakata la mchezaji Ramadhani Chombo 'Redondo', naomba
nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo. Redondo alipewa 'option' tatu za kuchagua baada
ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu timu ilipokuwa safarini Mwanza.
1. Kupelekwa kwa mkopo Moro United.
2. Kupatikana kwa mnunuzi mwenye Sh. milioni
40
3. Kukubali adhabu ya kufungiwa kwa miezi
mitatu na kulipwa nusu mshahara wahati akitumikia adhabu.
Redondo alithibitisha
kuipenda Azam FC kwa kukataa kuuzwa au kupelekwa kwa mkopo. Alikubali kutumikia
adhabu yake na ilipoisha alirudi na kuomba msamaha na sasa ni mmoja kati ya
wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu sana. Azam FC inajivunia kuwa na
mchezaji kama Redondo na bila kupepesa macho wala kung’ata maneno, Azam FC
inamchukulia Redondo kama mtu 'spesho' na mwenye mapenzi ya dhati na klabu yake
na inamtaka aendelee kuwa na moyo huo.
No comments:
Post a Comment