Straika Emmanuel Okwi wa Simba (kulia) akimtoka beki wa TP Mazembe katika mechi yao mojawapo ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. |
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akizungumza katika mkutano wao leo na kuwaambia wanachama kuwa wako tayari kumuachia Okwi kwa Yanga ikiwa watalipwa dola za Marekani milioni 2 (Sh. bilioni 3)! |
Katika kile
kinachoonekana kuwa ni kutaka kuwakomoa mahasimu wao wa jadi, Yanga, klabu ya
Simba imetangaza kuwa tayari kumuuza straika wao Emmanuel Okwi kwa dau kufuru la
dola za Marekani milioni 2, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 3.
Bei hiyo ya Okwi kwa
Yanga inazidi mara 13 ya kiasi cha pesa walichokihitaji Simba wakati wakimuuza
straika wao Mbwana Samatta kwenda klabu tajiri ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ilikuwa ni dola za Marekani 150,000 tu, sawa na Sh.
milioni 230!
Mwenyekiti wa Simba,
Ismail Aden Rage, ndiye aliyetangaza dau hilo linaloonekana wazi kuwa na dhamira
ya kufuta ndoto za Yanga kumtwaa Okwi wakati akizungumza kwenye mkutano wa
klabu hiyo ya Msimbazi uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Bwalo la Mafisa wa
Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Aidha, dau hilo la
Okwi pia linazidi takriban mara mbili ya bajeti ya Simba kwa mwaka ujao wa
fedha ambayo ilisomwa jana kwenye mkutano huo na kukadiriwa kuwa haitazidi Sh.
bilioni 1.6.
Rage alisema kuwa
Okwi bado ni mchezaji halali wa klabu yao na kama Yanga wanamuhitaji kweli,
basi watoe fedha taslim kiasi cha dola za Marekani milioni 2 (Sh. bilioni 3).
Hata hivyo, inakumbukwa
kwamba ni wiki iliyopita tu, Simba ilisema kuwa inatarajia kumuuza Okwi kwa euro
600,000 (sawa na Sh. bilioni 1.1) kwa mabingwa wa Austria, klabu ya Redbull
Salzburg ambayo ilishiriki hivi karibuni ilitoka kushiriki hatua ya awali ya
Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Viwango tofauti vya
bei ya mchezaji huyo, vinamaanisha kwamba Simba iko tayari kumuuza Okwi kwa bei
poa Ulaya kuliko kumuona anajiunga na Yanga; na kwamba thamani ya straika huyo
wa kimataifa wa Uganda ni mara 13 ya Mbwana Samatta waliyemuuza kwa TP Mazembe.
Akieleza zaidi kwenye
mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama zaidi ya 700, Rage alisema kuwa kwa
vyovyote vile, Okwi hawezi kukataa ofa ya mshahara wa euro 30,000 (sawa na Sh.
milioni 57) kwa mwezi nchini Austria na kujiunga na watani zao, Yanga ambao
wanasemekana wako tayari kumlipa mshahara wa Sh. milioni 2.5 kwa mwezi endapo
atakubali kujiunga nao.
No comments:
Post a Comment