Patrick Ochan |
NYOTA wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mganda Patrick Ochan, ametumia ukurasa wake wa facebook kuwashukia waliomsema vibaya kuelekea mechi yao ya jana ya Ligi uya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri ambayo walishinda 2-0 kwenye uwanja wa nyumbani wa TP Mazembe mjini Kinshasa.
Ochan alionekana kulalamikia ripoti za nchini kwao Uganda kwamba alikuwa amefungiwa kucheza.
"Jamani shukrani kwa sapoti mliyonipa leo tulipokuwa tukicheza dhidi ya Zamalek na asante Mungu tumeshinda 2-0. Natumai wale walioandika mabaya kuhusu mimi wameshuhudia mechi kwa sababu ilikuwa ikirushwa 'live' kwenye Supersport 9, sijui kama mchezaji aliyefungiwa anaweza kucheza. Wanachokifanya ni kutaka kuua soka la Uganda lakini pia samahanini kama kuna niliyemuumiza kwa sababu hata mimi nimeshawasamehe (walionisema vibaya) ni sehemu ya maisha lakini wakati mwingine tafuta ukweli kwanza kabla ya kurusha mambo hewani kwa sababu leo mimi kesho ni mchezaji mwingine. Hii ni kwa ajili manufaa ya (timu ya taifa ya Uganda) The Cranes kwa sababu ni ya Wauganda wote."
Nyota wa zamani wa klabu ya Simba, Ochan, aling'aa katika mechi hiyo ambayo alianza katika kikosi cha kwanza kabla ya kuja kupumzishwa katika dakika ya 65. Wakati akipumzishwa matokeo yalikuwa bado ni 0-0.
Kasongo aliifungia TP Mazembe goli la kuongoza katika dakika ya 70 na dakika nane baadaye mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (19) aliifungia klabu hiyo inayomilikiwa na bilionea wa madini, Moise Katumbi, goli la pili kwa kichwa kufuatia mpira wa 'fri-kiki' kutokea kushoto mwa uwanja.
TP Mazembe itaenda Misri wiki mbili zijazo kwa ajili ya mechi yao ya marudiano.
No comments:
Post a Comment