Friday, August 24, 2012

MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA 2012 YAFUTWA

Mshambuliaji wa timu ya Mkoa wa Mbeya, Gaudence Mwaikimba akipambana na beki wa Ruvuma, Abdallah Ausi wakati wa mechi ya robo fainali ya tatu ya mashindano ya Kili Taifa Cup iliyofanyika mwaka jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Mbeya ilishinda 3-2 na kutinga nusu fainali Mei 23, 2011.

MICHUANO ya Kombe la Taifa (Taifa Cup) inayoshirikisha kombaini za mikoa ya Tanzania Bara haitakuwepo mwaka huu kutokana na kukosekana kwa udhamini.

Taarifa iliyotolewa leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa afisa habari wake, Boniface Wambura, imesema licha ya kukosekana kwa udhamini, awali TFF ilifikiria kuendesha mashindano hayo kwa michango ya wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa) na Serikali za mikoa kugharamia timu zao.

"Lakini baadhi ya wanachama wetu na Serikali za mikoa walitushauri kuwa ni ngumu kuendesha mashindano hayo kwa sasa kutokana na shughuli za kitaifa zinazoendelea hivi sasa ikiwamo maandalizi ya sensa ya watu na makazi," ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya TFF, mashindano ya Kombe la Taifa yalitakiwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 6 mwaka huu.

Michuano ya Kombe la Taifa msimu uliopita ilidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambapo Mbeya iliibuka mabingwa katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment