Kila mechi Sh. 500, ukiwa na pungufu unaongea.... bango linaloonyesha mechi za leo kwenye ukumbi wa Old Trafford uliopo eneo la Tandika Maguruwe jijini Dar es Salaam. |
Mashabiki wa soka katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam hawana namna nyingine ya kuangalia mechi za klabu zao za soka za majuu kama England isipokuwa ni kwa kupitia vibanda maarufu vinavyoonyesha mechi hizo na filamu kwa bei poa, almaarufu kwa jina la "vibandaumiza".
Wapo wanokwenda kwenye maeneo ya 'kilaji' na kulazimika kununua vinywaji ili wapate nafasi ya kufuatilia mechi hizo kupitia vituo vya televisheni za kulipa. Hata hivyo, "vibandaumiza" ndio mkombozi kwa wakazi wengi wa maeneo ya "uswazi" kama Tandika, Yombo, Mbagala, Gongolamboto, Manzese, Kigogo, Mwananyamala, Buguruni, Msasani, Kinondoni, Ubungo, Mburahati, Chanika, Tabata, Mbezi, Kimara, Kigamboni, Tegeta, Mabibo, Buguruni, Magomeni Kagera, Vingunguti na kwingineko ambako wakazi wake wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kufunga 'ungo' na kulipia gharama za kila mwezi za huduma kama za kituo cha DSTV, kupitia chaneli zao za Super Sport zilizomo kwenye kifurushi cha PREMIER.
Kumbi hizi zisizo rasmi katika mitaa ya uswazi huitwa "vibandaumiza" kwa sababu watu hurundikana sana na kubanana kama ndizi, wakipumua kwa shida katika muda mwingi wa mechi. Pamoja na adha yake, ikiwemo ya harufu ya jasho, vikwapa na midomo itokanayo na wingi wa watu wanaoshangilia mfululizo na kunyeshea wenzao mvua ya mate; bado watumiaji wake wengi hujisikia poa tu.
Wateja hulipa senti kidogo za kuanzia Sh.200, Sh.300 hadi Sh.500 kulingana na ukubwa wa mechi, mahala kilipo "kibandaumiza" na upatikanaji wa nishati ya umeme katika siku husika. Mwishowe mashabiki hawa wa soka hufaidi uhondo wa mechi kali za soka za kimataifa kwa idadi waitakayo, hasa za klabu za Ligi Kuu ya England na La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa klabu za Barcelona na Real Madrid.
Ndani ya "vibandaumiza" vingi, utamu huongezeka kutokana na ubishi unaosababishwa na ukweli mmoja tu, nao ni ule wa kila shabiki kujifanya mchambuzi wa soka kupitia taarifa mbalimbali wanbazozipata kwenye magazeti, televisheni, redio na mitandao maarufu ya soka kama straikamkali.blogspot.com.
Wamiliki wengine wa hivi "vibandaumiza" wamekuwa wajanja zaidi na kuweka "dikoda" zaidi ya moja. Hatua hii huwapa fursa wateja wao kushuhudia mechi zaidi ya moja ambazo hugongana ratiba kwa kuchezwa kwa wakati mmoja; wakiweka skirini nyingi ukumbini kulingana na mahitaji.
Hakika, mgeni yeyote kutoka kutoka maskani za "kishua" jijini Dar es Salaam kama Oysterbay, Masaki na Mikocheni B, anaweza asiamini kile anachokishuhudia pindi anapokwenda kwenye kumbi hizi hasa katika mechi kubwa kama za "el clasico" kati ya Barcelona na Real Madrid au "derby" kama za Manchester United na Manchester City, Inter Milan dhidi ya AC Milan na hata Arsenal dhidi ya Manchester United. Lakini kwa wakazi wa maeneo husika ya uswazi, "vibandaumiza" ndio kila kitu.
Memba wake hujihisi furaha mno wanapotazama soka katika kumbi hizi zilizoshona watu na hivyo si ajabu, kwa mfano, shabiki wa soka wa Tandika Maguruwe akaacha kutazama mpira katika eneo tulivu la sebuleni akiwa na watu wengine wasiozidi watatu na kwenda kwenye "kibandaumiza" maarufu cha eneo lao kinachoitwa Old Trafford ili kufaidi raha za kubishana, kuzomeana, kuchekana, kupakiana mitusi na kushangilia ushindi kwa kelele kubwaaaaaaaa....!!
No comments:
Post a Comment