Friday, August 24, 2012

MATONYA OMBAOMBA AFARIKI DUNIA

Matonya enzi zake akiwa katika shughuli yake ya kuomba
Hamna mtu aliyekuwa akielewa ni wapi alipata mbinu hii ngumu na vipi aliimudu katika mazingira magumu, lakini Matonya aliomba kwenye jua kwenye mvua mchana kutwa akiwa amelala chini mikono juu. Mungu amlaze pema.


OMBAOMBA maarufu nchini, Matonya, amefariki dunia leo kijijini kwao Mpamantwa, wilayani Bahi mkoani Dodoma.

Matonya aliyepata umaarufu mkubwa kwa staili yake ya kuomba katika miji ya Dar es Salaam na baadaye Morogoro akiwa amelala chini huku amenyanyua juu kopo lake la kuombea fedha, amezikwa jirani na nyumba ya tembe aliyokuwa akiishi na mkewe wa tatu, Paulina Yohana.

Tofauti na ilivyokuwa ikidaiwa kwamba Matonya alikuwa na utajiri mkubwa kijijini kwao, familia yake haikuwa hata na fedha za kutengenezea jeneza la kuhifadhia mwili wake wakati akizikwa na walilazimika pia kufupisha shughuli za matanga.

Mtoto wanne wa Matonya, David Paulo alisema kwamba walishindwa hata kumpeleka hospitali kwavile hawakuwa hata na nauli ya kuwafikisha mjini Dodoma hivyo wakawa wakiomba Mungu tu mpaka alipokata roho.

Paulo alisema baba yake alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa kifua ambapo alikuwa akikohoa tangu Mei mwaka huu, na tangu wakati huo hawakuweza kumsaidia.

Paulina Matonya, mke wa marehemu, alisema wakati fulani miaka 37 iliyopita alitengana na mumewe na wakati huo hakuwa masikini kwani alikuwa na ng’ombe wengi.

Mama huyo amesema kwamba walipotengana ambapo yeye alirejea nyumbani kwao akiambatana na watoto wao, ng'ombe wote wa Matonya waliibwa kufuatia kifo cha mdogo wa Matonya ambaye alikuwa akiwatunza.

Licha ya kufahamika kwa jina la Matonya, ombaomba huyo ambaye aliingia jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7, 1961, jina lake la ubatizo ni Paulo Mawezi. Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu tisa.

Jina la Matonya limekuwa likitumika kuelezea mtu anayeombaomba kufuatia umaarufu na Matonya, ambaye alikuwa akipingana na serikali kuhusu kurudishwa makwao kwa watu wanaoomba mitaani agizo lililokuwa likitekelezwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Makamba.

Hata hivyo, baada ya kuhamishwa kutoka katika maeneo ya katikati ya Dar es Salaam, Matonya alihamia katika eneo la Darajani Morogoro.

No comments:

Post a Comment