Friday, August 24, 2012

ITC ZA KINA TWITE, AKUFFOR, KAVUMBAGU, MUDE ZATUA TFF... OCHIENG, KINJE MAMBO SI MAMBO SIMBA

Mshambuliaji Didier Kavumbagu (kushoto) akiwa na kocha Tom Saintfiet wa Yanga
Pascal Ochieng wa pili kulia) akitambulishwa Simba na Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange 'Kaburu' (wa pili kulia) na Zakaria Hanspope (kushoto) huku Daniel Akuffor (kulia) akishuhudia wakati wa Simba Day. Akuffor amepata ITC wakati Ochieng mambo yake bado magumu kwani klabu yake ya AFC Leopards imesema bado ina mkataba naye.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji 11 wa nje kati ya 14 walioombewa usajili na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Bara.
 

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, ameiambia STRAIKA kuwa jijini Dar es Salaam leo kuwa wachezaji walioombewa usajili Yanga na tayari ITC zao zimepatikana ni Mbuyu Twite kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Didier Kavumbagu (Atletico Olympic- Burundi) na Nizar Khalfan kutoka Vancouver Whitecaps ya Canada.

Kwa upande wa Simba ni Musa Mude (Sofapaka, Kenya) na Daniel Akuffor (Stella Abidjan, Ivory Coast) wakati Mtibwa Sugar ni Shabani Kisiga timu ya El Itihad ya Oman.

Waliopata ITC kwa upande wa Kagera Sugar ni Wilfred Ojodale Ame na Benjamin Efe Ofuyah wote kutoka FC Abuja ya Nigeria. Wengine ni Deangelis Silva kutoka New Road ya Nepal kwenda Coastal Union, George Odhiambo kutoka Randers FC ya Denmark kwenda Mtibwa Sugar na Jerry Santo kutoka Tusker, Kenya kwenda Coastal Union.

Wachezaji ambao wameombewa usajili na ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng wa AFC Leopards, Kenya kwenda Simba na Ayoub Hassan Isiko kutoka Bull FC, Uganda kwenda Mtibwa Sugar.

Bado klabu ambazo hazijakamilisha usajili na kupata ITC zina fursa ya kufanya hivyo hadi Septemba 4 mwaka huu ambapo dirisha litafungwa.

Pia TFF imetoa ITC kwa wachezaji wanane walioombewa kwenda kucheza mpira wa miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji kutoka katika klabu mbalimbali za hapa nchini.

Wachezaji hao na klabu wanazokwenda katika mabano ni Abdallah Ally Abdallah (CD Madchegde, Msumbiji), Almasi Khatib Mkinda (Ferroviario da Beira, Msumbiji), David Naftali (Bandari, Kenya) na Hassan Hassan Mustafa (CD Madchegde, Msumbiji).

Wengine ni Meshack Abel (Bandari, Mombasa), Mohamed Banka (Bandari, Kenya), Thobias Davis Silas (CD Madchegde, Msumbiji) na Thomas Maurice (Bandari, Kenya).

No comments:

Post a Comment