Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka. |
Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Kabaka |
Wabunge wamepiga kura nyingi za kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Suleiman Jaffu, aliyetaka kipengele hicho kinachozuia wafanyakazi kuchukua fao la kujitoa kifutiliwe mbali; akipendekeza kufanyika kwa utaratibu wa Serikali kurejesha bungeni mara moja muswada wa sheria hiyo ili hatimaye wabunge wajadili kipengele hicho kwa maslahi ya wananchi walio wengi, hasa wafanyakazi.
Mhe. Jaffu alitoa hoja hiyo jioni hii baada ya Bunge kukamilisha zoezi la kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka ujao wa fedha na Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda kumpa nafasi ya kuiwasilisha.
Aliposimama, Mhe. Jaffu aliyekuwa akishangiliwa na wabunge wa CCM na upinzani, alitoa mapendekezo kadhaa kuhusiana na maslahi ya wafanyakazi, kubwa likiwa ni pendekezo la kutaka wafanyakazi wote wapewe namba ya kuwatambua kama walipa kodi (TIN) kutokana na makato ya kila mwezi katika mishahara yao na pia kuondoshwa kwa kipengele cha kuzuia uchukuaji wa fao la kujitoa kinacholalamikiwa na wafanyakazi nchini kote na kuzua taharuki kubwa miongoni mwao.
Mhe. Jaffu alipomaliza kutoa hoja yake, Spika Makinda aliruhusu upigaji kura kwa kuwauliza wanaouunga mkono hoja ya Jaffu waseme "Ndiyo", ambapo wabunge wengi walijibu kwa kauli moja ya "Ndiyoooooooo...!"
Waliopinga hoja hiyo kwa kusema "Siyo" walikuwa wachache na hivyo hoja ya Jaffu ikapita na kuibua shangwe nyingi kutoka kwa wabunge waliokuwa wakipiga meza mfululizo baada ya spika kusema kuwa wanaounga mkono wameshinda.
Akitoa ufafanuzi baada ya tukio hilo, Spika Makinda alisema suala la kuletwa tena bungeni kwa muswada wa sheria ya mifuko ya hifadhi ili upitiwe upya litafanyika katika vikao vya Bunge la tisa kwani muda uliopo sasa hautoshi.
Hata hivyo, akaongeza kuwa, anaamini Serikali itatoa maelezo zaidi kesho wakati Waziri wa Kazi na Ajira atakapowasilisha hotuba ya makadario ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.
Hivi karibuni, wafanyakazi katikam maeneo mbalimbali nchini walitishia kuandamana ili kupinga sheria hiyo iliyopitishwa na bunge April mwaka huu na kusainiwa na rais hivi karibuni.
Awali, SSRA kupitia kwa mkurugenzi wake Irene Isaka ilitangaza kwamba kuanzia Julai 20 mwaka huu, wafanyakazi hwaruhusiwi tena kuchukua fao la kujitoa kazini kabla hawajatimiza miaka 55 ambao ni umri wa kustaafu na miaka 60 ambao ni umri wa kustaafu kwa lazima.
Wafanyakazi kadhaa wa migodini walipinga sheria hiyo kwa kuitisha mgomo na kutaka kuandamana, huku wakiwazomea kupita kawaida maafisa wa SSRA waliowaendea na kujaribu kuwapoza.
No comments:
Post a Comment