Monday, August 13, 2012

FABREGAS AMCHANA PEP GUARDIOLA, ADAI MFUMO WAKE ULIMSHINDA ND'O MANA AKAONEKANA NYANYA

Cesc Fabregas
Fabregas akisindikizwa na kocha Guardiola kuingia uwanjani akitokea benchi katika mechi yao ya kuwania taji la 'Super Cup' dhidi ya Real Madrid iliyochezwa Agosti 17, 2011. 
Kocha Guardiola akiwapongeza wachezaji wake Fabregas na Javier Mascherano baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 4-3 katika mechi yao ya marudiano ya kuwania taji la 'Super Cup' dhidi ya Real Madrid Agosti 17, 2011. 
MADRID, Hispania
CESC Fabregas amekiri kwamba alipata wakati mgumu sana kuzoea uchezaji wa Barcelona msimu uliopita kwa sababu ya mfumo wa uchezaji uliokuwa ukitumiwa na kocha Pep Guardiola.

"Chini ya Guardiola sikuwahi hata mara moja kuuzoea mfumo wa uchezaji," kiungo huyo mwenye miaka 25 alikaririwa akisema kwenye gazeti la Marca leo.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania alihama Arsenal na kutua Barca katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2011, lakini alikuwa na wakati mgumu kuonyesha kiwango alichotarajiwa ambapo sasa amesema kwamba kutocheza kwa uhuru kutokana na mfumo wa Guardiola ndiko kulikomponza na kumfanya aonekane 'amechemsha'.

"Nilikuwa nikicheza mtindo mwingine wa soka na hivyo kuzoea mfumo mwingine kwa haraka ilikuwa kazi ngumu sana kwangu, hasa kwa vile wenzangu wote walikuwa wameshauelewa," Fabregas alieleza.

Aliongeza, "Kucheza katika nafasi ya kiungo ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nahitaji kuzunguka zaidi na mimi sio mwepesi sana kiasi cha kucheza katika eneo la mita chache kunizunguka.

"Sihitaji chochote, lakini hiyo ndiyo aina yangu ya kucheza. Ni kweli kwamba kwa kiasi fulani sina mpangilio maalum, lakini huo nd'o uchezaji wangu. Baadhi ya watu walisema kwamba kuna kitu nilikikosa msimu uliopita, akiwemo Guardiola."

Fabregas amekiri kwamba alianza msimu uliopita kwa kujaribu kucheza kama viungo wengine aliowakuta Barcelona.

"Kwakweli hilo lilikuwa kosa langu kwa sababu nilijaribu kuonekana kwa namna isiyoendana na mimi; mimi sio Xavi, (Andres) Iniesta, au Thiago (Alcantara). Mimi ni mimi na ninahitaji kuzunguka huku na kule uwanjani, kucheza zaidi ya eneo moja."

Fabregas alifunga mabao tisa katika mechi 28 za La Liga alizocheza msimu uliopita. Hivi sasa, Barca inaongozwa na kocha Tito Vilanova aliyerithi mikoba ya Pep Guardiola aliyeamua kutosaini mkataba mwingine baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment