Monday, August 27, 2012

AZAM YAUA 8-0, BOCCO ATUPIA 2


Na Mwandishi Wetu
KUSHINDWA katika majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, hakukumzuia John Bocco 'Adebayor' kuendeleza makali yake ya kufumania nyavu katika soka la Bongo wakati alipofunga magoli mawili na kuisaidia timu yake ya Azam FC kuibuka na ushindi mnono wa 8-0 dhidi ya Transit Camp ya Ligi Daraja la Kwanza katika mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Bocco alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Super Sport United inayoshiriki Ligi Kuu ya huko, aliingia katika fainali ya kuwania nafasi moja ya pamoja na wachezaji wengine wawili kutoka Nigeria, lakini alikosa nafasi hiyo na kurejea nchini.

Katika mechi hiyo ya kirafiki, mfungaji bora wa ligi kuu ya Bara msimu uliopita Bocco alifunga magoli mawili sawa na Gaudence Mwaikimba na mshambuliaji mwingine, Papie, aliye katika majaribio, wakati Kipre Tchetche na Abdulhalim Humoud kila mmoja alifunga bao moja.

Azam ambao wataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Shirikisho mwakani, iliitumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mechi yake ya Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa, Simba, itakayochezwa wiki moja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.

Mechi ya Ngao ya Jamii mwaka jana ilikutanisha watani wa jadi na Simba ilibeba ngao baada ya kuifunga Yanga magoli 2-0 kupitia kwa Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu.

Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii itakuwa ni mtihani wa pili kwa kocha mpya wa Azam, Mserbia Boris Bunjak 'Boca' baada ya kufungwa na Simba B hivi karibuni kwenye michuano ya Super8.

No comments:

Post a Comment